• HABARI MPYA

  Sunday, November 05, 2023

  RAIS DK SAMIA AWAPONGEZA YANGA KWA USHINDI MNONO DHIDI YA SIMBA  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amewapongeza Yanga kwa ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya mahasimu wa jadi, Simba SC.
  “Hongereni Yanga kwa ushindi dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Upinzani wenu wa jadi wa zaidi ya miaka 85 sasa ni sehemu muhimu ya burudani yetu. Mnawaleta pamoja na kwa namna kipekee, mamilioni ya Watanzania ndani na nje ya nchi yetu,” amesema
  Mheshimiwa Rais Dk. Samia katika ukurasa wake wa Instagram jioni hii.
  Mabingwa watetezi, Yanga SC wamewaadhibu ipasavyo watani wa jadi, Simba kwa kuwatandika mabao 5-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara leo Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Mabao ya Yanga leo yamefungwa na mshambuliaji Mzambia, Kennedy Musonda dakika ya tatu na viungo, Mkongo Maxi Mpia Nzengeli dakika ya 64 na 77, Mburkinabe Stephane Aziz Ki dakika ya 73 na Muivory Coast Pacome Zouazoua dakika ya 87 kwa penalti.


  Refa Ahmad Arajiga wa Manyara alitoa adhabu ya penalti baada ya beki Mkongo, Henock Inonga Baka ‘Varane’ kumchezea rafu Nzengeli kwenye boksi na bao pekee la Simba limefungwa na Kibu Dennis Prosper dakika ya tisa.
  Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 21 katika mchezo wa nane na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu, ikiizidi pointi mbili Azam FC ambayo pia imecheza mechi moja zaidi.
  Kwa upande wao, Simba SC baada ya kipigo hicho cha kihistoria, inabaki na pointi zake 18 za mechi saba nafasi ya tatu.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RAIS DK SAMIA AWAPONGEZA YANGA KWA USHINDI MNONO DHIDI YA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top