• HABARI MPYA

  Tuesday, November 28, 2023

  BENCHIKA APEWA MIAKA MIWILI SIMBA SC, AAHIDI KUREJESHA MSIMBAZI


  KOCHA mpya wa Simba SC, Mualgeria Abdelhak Benchikha ameahidi kurejesha furaha kwa mashabiki wa timu hiyo baada ya kujunga na Wekundu hao wa Msimbazi kwa mkataba wa miaka miwili.
  Benchika aliyetambulishwa rasmi leo kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam amesema kwamba amefurahi kujiunga na Simba, kwania tangu alipoanza mawasiliana na uongozi wa klabu juu ya dili hilo alikuwa ana shauku ya kuja. 
  Benchika ambaye msimu uliopita aliipa USM Alger ya kwao ubingwa wa Kombe la Shirkisho Afrika akiizidi kete Yanga kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya kushinda 2-1 Dar es Salaam na kufungwa 1-0 Algiers amesema kwamba jambo kubwa ambalo anaomba ni mashabiki kumpa ushirikiano na anaamini kupitia hilo watafanikiwa pamoja.
  “Kuna mambo mengi ambayo tayari nayajua na nimekuja na mikakati ambayo tayafanyia kazi. Kuhusu wachezaji nitajua zaidi nikishaanza kazi, kuhusu mashindano ya ndani na kimataifa yote ni muhimu. Mimi ni mpambanaji na nitapambana hadi tutafika,” amesema na kuongeza;
  “Mafanikio yatajengwa na Wanasimba wote hilo ndio muhimu zaidi. Kwa wachezaji sitaangalia majina bali anayefanya vizuri, kiwango cha mchezaji ndio kitafanya nimtumie.”
  Mapema katika mkutanohuo, Mtendaji Mkuu wa Simba SC Imani Kajula alisema kwamba haikuwa jambo rahisi kumpata Kocha Benchika mwenye rekodi ya mafanikio kuanzia ngazi ya klabu hadi timu za taifa za Algeria kuanzia za vijana hadi ya wakubwa alizofundisha.
  "Lengo letu kama klabu tulitaka mwalimu ambaye atatupeleka mbali. Kumpata mwalimu mzuri ni mchakato mkubwa sana. Mwalimu Benchikha atakuwepo kwa mkataba wa misimu miwili. Bodi ya Simba, menejimenti ya Simba imempa mwalimu uhuru wa kufanya kazi. Sisi ni moja ya klabu bora Afrika hatuwezi kufanya kazi kwa kumbana,” amesema Kajula.
  Benchika amekuja na Wasaidizi wawili, Kocha Msaidizi Farid Zemiti na Kocha wa Utimamu wa Mwili (Fitness), Kamal Boudjenane ambao alikuwa nao wakati anatwaa Kombe la Shirikisho akiwa USM Alger pamoja na Super Cup ya Afrika kwa kuifunga Al Ahly ya Misri. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BENCHIKA APEWA MIAKA MIWILI SIMBA SC, AAHIDI KUREJESHA MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top