• HABARI MPYA

  Jumatano, Novemba 25, 2020

  KASEKE AFUNGA BAO PEKEE CHAMAZI YANGA SC WAICHAPA AZAM FC 1-0 NA KUPANDA KILELENI LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu,  DAR ES SALAAM
  VIGOGO, Yanga SC wamepanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Azam FC leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
  Shujaa wa Yanga SC ni leo ni kiungo wake, Deus Kaseke aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 48 akimchamba kwa mguu wa kulia kutoka umbali wa mita 14 kipa David Mapigano Kissu kufuatia pasi maridadi ya mshambuliaji Mburkinabe, Yacpouba Sogne. 
  Refa Emmanuel Mwandemba aliyesaidiwa na Charles Simon na Kassim Mpanga aliwaonyesha kadi za njano mabeki Mghana Lamine Moro wa Yanga SC, Mganda Nico Wadada na mshambuliaji Muivory Coast, Richard Ella D’jodi wa Azam FC kwa makosa tofauti.
  Na kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 28 na kupanda kileleni, ikiwazidi pointi tatu Azam FC baada ya timu zote kucheza mechi 12 – wakiwa mbele ya mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 23 za mechi 11.  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo; Ruvu Shooting imeichapa 1-0 Tanzania Prisons, bao pekee la Abrahman Mussa dakika ya 30 Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. 
  Nayo Kagera Sugar ikailaza 3-0, mabao ya Erick Mwijage dakika ya 10, Nassor Kapama dakika ya 77 na Hassan Mwaterema dakika ya 79 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. 
  Nayo Gwambina FC ikaibuka na ushindi wa ugenini wa 4-3 dhidi ya jirani zao, Mwadui FC Uwanja wa Mwadui Complex, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga. 
  Mabao ya Gwambina yamefungwa na Jimson Stephen dakika ya sita, Jacob Massawe dakkika ya 26 na 66 na Meshack Abraham dakika ya 45, wakati ya Mwadui FC yamefungwa na Herman Masenga dakika ya 15, Salum Chuni dakika ya 39 na Ismail Ally dakika ya 62. 
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; David Kissu, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Daniel Amoah, Ally Niyonzima, Never Tigere, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Prince Dube/Richard Ella D’jodi dk23, Mudathir Yahya/Alan Thiery Akono dk51 na Ayoub Lyanga/ Idd Suleiman ‘Nado’ dk63. 
  Yanga SC; Metacha Mnata, Kibwana Shomary/ Said Juma ‘Makapu’ dk56, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Tonombe Mukoko, Tuisila Kisinda, Feisal Salum, Deus Kaseke/Faris Mussa dk70, Ditram Nchimbi/Michael Sarpong dk66 na Yacouba Sogne.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KASEKE AFUNGA BAO PEKEE CHAMAZI YANGA SC WAICHAPA AZAM FC 1-0 NA KUPANDA KILELENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top