• HABARI MPYA

  Alhamisi, Novemba 26, 2020

  AZAM FC YAWATUPIA VIRAGO MAKOCHA WAKE WAROMANIA BAADA YA KIPIGO CHA YANGA SC JANA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Azam FC imefikia makubaliano ya kuachaana na kocha wake, Aristica Cioaba pamoja na Msaidizi wake mmoja, Kocha wa mazoezi ya viungo, Costel Birsan, wote raia wa Romania.
  Taarifa ya Azam FC leo imesema kwamba aliyekuwa Kocha Msaidizi, Mrundi Bahati Vivier ndiye atakayeiongoza timu kuanzia sasa hadi atakapopatikana kocha mwingine Mkuu.
  “Tunawashukuru Cioaba na Costel, kwa mchango wao chanya walioutoa kwa kipindi chote walichohudumu ndani ya timu hii na tunapenda kuwatakia kila la kheri popote watakapokwenda,” imesema taarifa ya Azam FC.
  Uamuzi huo unakuja siku moja baada ya Azam FC kufungwa 1-0 na Yanga SC, bao pekee la kiungo Deus Kaseke dakika ya 48 akimalizia pasi ya mshambuliaji Mburkinabe, Yacpouba Sogne katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. 

  Aristica Cioaba amefukuzwa Azam FC kwa pamoja na Msaidizi wake, Costel Birsan, wote Waromania 

  Matokeo yaliiondoa Azam FC kileleni, wakiipisha Yanga SC iliyofikisha pointi 28, ikiidi pointi tatu timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa  na familia yake baada ya timu zote kucheza mechi 12 – wakiwa mbele ya mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 23 za mechi 11. 
  Cioaba aliyekuwa anaiongoza Azam FC kwa awamu ya pili, tangu arejee ameiongoza timu hiyo kwenye mechi 50 za mashindano tofauti, akishinda 28, sare 11 na kupoteza 11.
  Awali aliiongoza Azam FC kuanzia Januari 10, 2017 hadi Mei 3, 2018 alipofukuzwa kabla ya kurejeshwa Oktoba 22, mwaka jana kufuatia kuondoka kwa Mrundi, Etienne Ndayiragijje aliyehamia timu ya taifa, Taifa Stars.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAWATUPIA VIRAGO MAKOCHA WAKE WAROMANIA BAADA YA KIPIGO CHA YANGA SC JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top