• HABARI MPYA

  Jumapili, Novemba 22, 2020

  METACHA MNATA AOKOA PENALTI DAKIKA YA MWISHO, YANGA SC YATOA SARE 1-1 NA NAMUNGO DAR

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MLINDA mlango, Metacha Boniphace Mnata leo ameinusuru klabu yake, Yanga SC kupoteza mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuokoa mkwaju wa penalti wa dakika ya mwisho wa Mrundi, Bigirimana Blaise timu hiyo ikitoa sare ya 1-1 na Namungo FC ya Ruangwa mkoani Lindi.
  Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam, Mnata aliuchupia mkwaju huo na kuupngua kaba ya kuuondosha hatarini na kuamsha shangwe za mashabiki wa timu ya Jangwani – wakishukuru kwa sare ya nyumbani kuliko kupoteza mechi.
  Penalti hiyo ilitolewa na refa Raphael Ikambi kutoka Morogoro baada ya beki muhimili wa safu ya ulinzi ya Yanga, Bakari Nondo Mwamnyeto kumuangusha winga wa Namungo FC, Shiza Ramadhani Kichuya kwenye boksi. 
  Yanga SC ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao leo mapema tu dakika ya 13, mfungaji kiunho Muangola, Carlos Carlinhos akimalizia kwa kichwa krosi ya beki wa kulia, Kibwana Shomari.
  Lakini bao hilo halikudumu sana, baada ya mshambuliaji Mghana, Steven Sey kuisawazishia Namungo FC dakika ya 16 akinufaika na makosa ya kiungo Farid Mussa Malik.   
  Kwa matokeo hayo, Yanga SC inafikisha pointi 25, ingawa inabaki nafasi ya pili ikizidiwa wastani wa mabao na Azam FC baada ya timu zote kucheza mechi 11, sawa na mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 23. 
  Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, bao pekee la Hassan Materema dakika ya 63 limeipa Kagera Sugar ushindi wa 1-0 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Tonombe Mukoko, Tuisila Kisinda/Ditram Nchimbi dk71, Feisal Salum, Michael Sarpong, Carlos Carlinhos na Farid Mussa/Deus Kaseke dk55.
  Namungo FC; Jonathan Nahimana, Miza Chrstom/Haruna Shamte dk69, Edward Manyama, Hamisi Mgunya, Carlos Protas, Khamis Khalifa, Sixtus Sabilo/Iddi Kipagwile dk58, Freddy Tangalo, Steven Sey/Shiza Kichuya dk83, Lucas Kikoti na Bigirimana Blaise.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: METACHA MNATA AOKOA PENALTI DAKIKA YA MWISHO, YANGA SC YATOA SARE 1-1 NA NAMUNGO DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top