• HABARI MPYA

    Saturday, November 21, 2020

    BURIANI KAPTENI MALIKI FAKI, MTU MUHIMU KATIKA HISTORIA YA YANGA

    Na Dk Ramadhani Kitwana Dau, DAR ES SALAAM
    JUMATANO ya tarehe 11 Novemba 2020 ni siku ambayo soka la Tanzania limepatwa na pigo kubwa kwa kuondokewa na mmoja wa watu waliohifadhi kumbukumbu nyingi sana kuhusu soka la Afrika Mashariki.
    Ilikuwa saa 4 na dakika 2 usiku kwa saa za Malaysia (saa 11 na dakika 2 jioni kwa saa za Tanzania) wakati mwanangu Ahmad Ramadhani Dau aliponitumia ujumbe mfupi uliosema “Assalaam Alaykum. Captain Malik amefariki”. Mara tu nilipopata ujumbe huo nikajua kuwa umeniangukia wajibu wa kuandika Taazia ya kumuenzi Captain Maliki pamoja ya kuwa kuandika Taazia si jambo ambapo nalifurahia kwa sababu ambazo nimeshazieleza huko nyuma. Lakini Waswahili wanasema “lisilobudi hutendwa”. Kwa kuwa hii si mara yangu ya kwanza kuandika Taazia, mrejesho (feedback) ambao nimekuwa nikipata kutoka kwa wasomaji mbalimbali na hata baadhi ya Wahariri ni kuwa Taazia zangu ni ndefu sana. Kwa sababu hiyo, Taazia hii itakuwa fupi ingawa kwa kufanya hivyo ninajua kuwa nitawakosesha wasomaji mambo mengi ambayo marehemu Capt. Maliki aliwahi kunisimulia wakati wa uhai wake. 


    Captain Maliki alizaliwa tarehe 15 Oktoba 1936 kisiwa cha Kwale Wilaya ya Mkuranga (karibu na Kisiju). Alikuwa ni kati ya watoto wawili (yeye na dada yake Mgeni binti Faki Abdallah) wa Mzee Faki Abdallah na mkewe Bi Mwanaviwa binti Mwinyimadi Mkendwa. Ndugu zake wengine alizaliwa nao mama mmoja ambao ni: Mzee bin AbdulRahman bin Maalim, Yahya bin AbdulRahman bin Maalim, Mwanahamisi binti AbdulRahman bin Maalim, Amina binti AbdulRahman bin Maalim na Mwatumu binti AbdulRahman bin Maalim. Captain Maliki alikuja Dar es Salaam mwaka 1955 na alifikia Mwembetogwa (kwa jina la sasa hivi “Fire”), kwenye nyumba ya marehemu Thabit Iddi maarufu John Iddi (baba yake Iddi John). Kikazi, katika umri wake wote, Capt. Maliki aliajiriwa na Public Works Department (PWD) kama fundi wa vitasa vya milango. Mimi nilibahatika kumfahamu Capt. Maliki tokea nikiwa mtoto mdogo wa chini ya umri wa miaka 6 kwa sababu nilizaliwa, nilelewa na niliishi Mwembetogwa.  Wakati huo Capt. alikuwa akijulikana kwa jina la utani Dr. Nnamdi Azikiwe (maarufu “Zik”) ambaye alikuwa Rais wa Nigeria kati ya mwaka 1963-1966.
    Jina kamili la marehemu Capt. Maliki ni Maliki Faki Abdallah lakini kwa muda wote wa uhai wake alijulikana zaidi kama Capt. Maliki ingawa kwa watu wachache sana wakimjua pia kwa jina la Dr. Nnamdi Azikiwe. Marehemu Capt. Maliki alianza kujishughulisha na mpira akiwa mchezaji wa African Boys ambayo ilikuwa timu B ya Yanga (Young Africans).   Alikuwa namba 4 na nahodha wa timu na ndio sababu ya kupata jina la Captain. Akiwa mchezaji wa African Boys na baadae Yanga, Capt. Maliki alitoa mchango mkubwa sana haswa kwenye klabu ya Yanga kwa kuwaleta wachezaji ambao baadae walikuwa maarufu sana na wengine walichezea timu ya Taifa kwa miaka kadhaa. Baadhi ya wachezaji ambao Captain Maliki aliwashawishi na kuwafuata yeye mwenyewe kuwaleta Dar es Salaam kuchezea timu ya Yanga ni marehemu Athumani Kilambo (a.k.a Baba watoto, ambaye alimfuata Bagamoyo) marehemu Maulidi Bakari Dilunga (ambaye alijulikana kwa majina ya utani matatu, “Eusebio”, “Mexico” na “DDT” yaani Dilunga Dangerous Ten, alimfuata Mzumbe Sekondari alipokuwa anasoma), Abuu Marwa (baadae alikwenda kucheza Cosmopolitan), marehemu AbdulRahman Juma (a.k.a mapafu ya mbwa, kwa muda mrefu sana alikuwa Captain wa Yanga, Dar es Salaam combine na timu ya Taifa) Brian Segatwa, Semboko nk. Wengi kati ya wachezaji hao ndio waliokuwa msingi wa timu iliyoifunga Sunderland 5-0 mwaka 1968. 
    Mwenyezi Mungu Alimjaalia Capt. Maliki kipaji cha ajabu cha kutunza kumbukumbu ghibu. Alikuwa ana uwezo wa kupanga timu za Taifa za Kenya, Tanganyika, Uganda na Zanzibar za mashindano ya Gossage (baadae Challenge Cup) kwa miaka ya 1950, 1960 na 1970.   Hali ilikuwa ni hivyo hivyo kwenye timu za vilabu vya Cosmo, Simba, TPC, Yanga, nk. Uwezo wake haukuishia kwenye kupanga listi ya timu hizo, bali alikuwa na uwezo wa kusimulia jinsi mechi zilivyochezwa, timu gani ilivaa jezi ya aina gani, timu ziliingia uwanjani saa ngapi, timu ipi ilitangulia kuingia uwanjani, matokeo yalikuwa vipi, nani waliofunga magoli na katika dakika ya ngapi. Msemaji wa Simba Haji Sunday  Manara hakukosea aliposema mara kadhaa kuwa Capt. Maliki alikuwa  Encyclopedia ya mpira wa Afrika Mashariki. 
    Yapo mengi sana ambayo Dr. Nnamdi Azikiwe alinisimulia ambayo yanasisimua sana. Lakini kwa uhaba wa nafasi, leo nitasimulia kisa kimoja tu. Kwenye kisa hiki, Capt. Maliki alikuwa anajaribu kunionesha ni namna gani wapenzi wa mpira wa zamani walivyokuwa na mapenzi makubwa na timu zao tofauti na ilivyo hivi sasa. Captain anasimulia kuwa mwaka 1955/1956 kulikuwa na mechi baina ya Sunderland (sasa Simba) na Yanga. Wakati huo Sunderland ilikuwa ina mchezaji kiungo mshambuliaji hodari sana akiitwa Kilima Abdallah Huni ambaye pia alikuwa mchezaji wa timu ya Taifa ya Tanganyika.  Siku chache kabla ya mechi, Kilima akapatwa na kesi ambayo  baadhi ya watu waliitakidi kuwa alibambikiwa na wapenzi wa Yanga ili awekwe rumande au afungwe jela na akose kucheza mechi hiyo ambayo ilikuwa na ushindani mkubwa. Ikumbukwe kuwa miaka hiyo mechi ya Sunderland na Yanga ilikuwa inachezwa mara moja tu kwa mwaka. Kwa hiyo timu ikifungwa inabidi isubiri mwaka mzima kabla haijapata nafasi ya kulipiza kisasi. 
    Kesi ikapelekwa kwa Hakimu anaitwa Nassoro Kiruka, Mzee wa Kimanyema na mwanachama mkubwa wa Yanga na alikuwa akiogopwa sana. Mwanawe alikuwa anaitwa Selemani Kiruka mwanachama mwanzilishi wa Pan Africa Football Club. Wakati kesi inaendelea kusikilizwa ghafla aliinuka Bwana Yahaya Kiambwe (mwenyeji  wa Rufiji) ambaye alikuwa mshabiki mkubwa wa Sunderland na kumwambia Hakimu kuwa anaomba kesi ya Kilima apewe yeye na ikibidi afungwe yeye ili Kilima aachiwe huru kwa sababu kesho yake Sunderland inacheza na Yanga na Kilima ni mchezaji ambaye wanamtegemea sana kwenye mechi hiyo! Captain Maliki anasema mapenzi ya vilabu yalifikia hatua hiyo. Hatimaye Kilima aliachiwa huru na akacheza mechi dhidi ya Yanga. Capt. Maliki anasimulia kuwa mchezo ulikuwa mkali sana na wenye ushindani mkubwa haswa kwa vile washabiki wa Simba waliamini kuwa kulikuwa na njama za kumfanya Kilima akose mechi ile. Mpira ulipokwisha kuna timu ilishinda 1-0. Wakati naandika Taazia hii, kwa kupitia simu ya Mohamed Rishad (Adolf), nilizungumza na Bwana Yusuf Salum Maleta aliyekuwa beki wa kulia wa Sunderland akiwa nyumbani kwake Kinondoni, Mkwajuni.  Yeye alikithibitisha kisa hiki na kunitajia jina la mchezaji aliyefunga goli. Je ni timu ipi iliyoshinda? Nani alifunga goli? Fumbo hili nakuachia wewe msomaji. 
    Jambo ambalo limenisikitisha sana ni kuondoka Capt. Maliki bila kuacha urithi wake kwa kizazi cha sasa na vijavyo. Wakati wa uhai wake mimi na Mohamed Saidi tulimuomba sana aandike kumbukumbu hizo na Mohamed alijitolea kuifanya kazi hiyo kwa njia ya mahojiano na baadae aiweke vizuri katika mfumo wa kitabu. Kwa wale wote waliopata bahati ya kumjua na kuzungumza na Capt. Maliki kuhusu masuala ya mpira Afrika Mashariki wataelewa umuhimu wa kuweka kumbukumbu hizo kwa sababu baadhi ya mambo aliyokuwa anayazungumza huwezi kuyapata kwenye vitabu au nyaraka zozote.  Kwa mfano wapi unaweza kupata rekodi ya timu ipi ilitangulia kuingia uwanjani na kwa sababu gani, timu ipi iliingilia mlango gani na kwa sababu ipi, mchezaji yupi alitangulia kushuka kwenye gari, mchezaji yupi alitangulia kuingia uwanjani na alitanguliza mguu upi. Wapi leo utapata kumbukumbu inayoeleza kwa nini mechi ya Sunderland na Yanga iliyochezwa kwa mara ya kwanza uwanja wa Taifa (sasa uwanja wa Uhuru)  mwaka 1969, timu zote tatu (ndiyo ni timu tatu) zilifika uwanjani mapema lakini mchezo ulichelewa kuanza hadi saa 12 jioni? Kwa nini Maulidi Bakari Dilunga (Eusebio) alitoka nje mara tu baada ya kufunga goli dakika 15 za kipindi cha kwanza? Na kwa nini Dilunga aliambiwa na viongozi wa Yanga aondoke kabisa uwanjani aende nyumbani kwake Magomeni mtaa wa Ubungo wakati mechi inaendelea? Kwa mpira wa zamani hayo yote yalikuwa na sababu na umuhimu wake katika kutafuta ushindi lakini si rahisi kuyapata kwenye vitabu vya historia. Marehemu Capt. Maliki alikuwa anasimulia kisa hiki na visa vingine vingi utadhani vimetokea jana. Capt. Maliki pia ana kumbukumbu ya mwaka ambao klabu ya SIMBA ilikuwa na Makamu Mwenyekiti Juma NYATI na kocha kutoka Hungary John FARU. Pia alikuwa anakumbuka alichokisema mchezaji wa Brazil Pele kuhusu Maulidi Dilunga kuwaambia marehemu Johnson Mbwambo (Katibu Mipango wa Yanga) na marehemu Ibrahim Pazi (Mweka Hazina wa Yanga) walipokwenda Brazil kusaini Mkataba wa kuileta timu ya Santos (akiwemo na Pele) kuja Tanzania kama wageni wa Yanga. Bahati mbaya Captain Maliki hakuwahi kuzikusanya kumbukumbu zake kwa njia ya kitabu mpaka umauti ulipomfika na kurejea kwa Mola Wake. Ushauri kama huo nimempa Mohamed Rishad “Adolf” kwa sababu baada ya Capt. Maliki mtu mwingine mwenye kumbumbuku nzuri sana ni yeye. Lakini kwa jinsi ninavyomfahamu rafiki yangu huyu wa miaka 48 (tokea 1972) nina hakika hatofanya hivyo. 
    Jambo lingine la kusikitisha kufuatia msiba huu ni kukosekana kwa viongozi wa Yanga kwenye maziko ya Capt. Maliki. Nimesema ni jambo la kusikitisha (sio kwamba nawalaumu) kwa sababu kwa bahati mbaya viongozi wa Yanga na hata vilabu vingine vikongwe hawajui historia yao.  Nina hakika wanachama na hata viongozi wa Yanga wa sasa hawamjui Capt. Maliki alikuwa nani na alitoa mchango gani kwenye klabu yao. Hili limedhihiri kwangu kiasi miaka 4 au 5 iliyopita wakati niliposoma kwenye Gazeti la Yanga Imara ambalo nadhani ni Gazeti rasmi la klabu ya Yanga. Katika toleo hilo mwandishi amezungumzia mgogoro wa Yanga uliopelekea kuanzishwa kwa timu ya Pan Africa. Mwandishi amedai kuwa mgogoro huo ulianza mwaka 1973 wakati Yanga walipofungwa goli 1-0 kwa goli lilofungwa na Haidari (Muchacho) kufuatia kross ya Wellington Mwaijibe. Baada ya mechi hiyo ikazuka tafrani na hatimaye kuanzishwa timu ya Pan Africa. Hili sio kweli kabisa. Inashangaza sana kuona klabu kubwa kama Yanga inashindwa kuwa na historia sahihi ya maisha yake. Kama mgogoro wa Yanga ulianza 1973, je wakati wa mechi ya Simba na Yanga ya Nyamagana Mwanza Agosti 1974 timu ya Pan Africa ilikuwa wapi na nani walikuwa wanachezea timu hiyo?  Je wakati wa mechi ya Simba na Yanga Januari 1975 Zanzibar, timu ya Pan ilikuwa wapi? Na je Yanga ilipokwenda kutetea kikombe cha Afrika Mashariki Januari 1976 Mombasa, timu ya Pan ilikuwa wapi na nani walikuwa wachezaji wake? Majibu ya maswali yote hayo ni kwa timu ya Pan Africa ilikuwa haijaanzishwa! Mgogoro wa Yanga ulianza baada ya mechi ya Yanga na Enugu Rangers ya Nigeria mwezi Mei 1975. Habari yake ni ndefu na hapa si mahala pake. 
    Natoa wito kwa vilabu vikubwa viandike historia ya timu zao tokea zilipoanzishwa na zijenge utamaduni wa kuwaenzi watu waliotoa mchango mkubwa katika kuanzishwa na kuendelezwa kwa timu hizo. Bado muda upo kwa sababu baadhi ya wazee wenye kumbukumbu bado wapo hai na Mwenyezi Mungu Awape umri mrefu zaidi ili tuvune uzoefu na busara zao. Baadhi ya wazee hao ni mjomba wangu Jabiri Katundu (Yanga) mjomba wangu Akherina Katundu (Simba), Yusuf Salum Maleta (full back wa Sunderland), Mustafa Choteka (namba 10 Sunderland), Hamisi Kilomoni (half back Sunderland) Emmanuel Albert Mbele (Yanga baadae Simba center forward) Gilbert Mahinya (Sunderland baadae Yanga half back) n.k. Aidha natoa wito kama huo kwa TFF (ambapo mimi ni mmoja wa Wadhamini) waandike historia ya timu ya Taifa tokea wakati wa ukoloni hadi hivi sasa. 
    Buriani Capt. Maliki Fakih Abdallah a.k.a Dr. Nnamdi Azikiwe. Mwenyezi Mungu Ailaze roho yake mahala pema.   
    Innallillah Wainnaillahi Rajiuun.  Sisi sote ni Waja wa Mwenyezi Mungu, na Kwake Yeye ndio marejeo yetu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BURIANI KAPTENI MALIKI FAKI, MTU MUHIMU KATIKA HISTORIA YA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top