• HABARI MPYA

    Tuesday, January 07, 2020

    SIMBA YAICHAPA ZIMAMOTO 3-1 NA KUTINGA NUSU FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI, ITAIVAA AZAM

    Na Mwandishi Wetu, PEMBA
    SIMBA SC itakutana na Azam FC katika Nusu Fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi Ijumaa Uwanja wa Amaan, Zanzibar kuanzia Saa 2:15 usiku.
    Hiyo ni baada ya mabingwa hao wa Tanzania kuwatupa nje Zimamoto ya Zanzibar kwa kuwachapa mabao 3-1 jioni ya leo Uwanja wa Gombani, Pemba.
    Mabao ya Simba SC leo yamefungwa na Nahodha wake, mshambuliaji John Raphael Bocco dakika ya tano na viungo, Msudan Sharaf Eldin Shiboub dakika ya tisa na mzawa, Ibrahim Ajibu dakika ya 54, wakati bao pekee la Zimamoto limefungwa na Ibrahim Ahmad ‘Hilika’ dakika ya 29.


    Azam FC yenyewe ilitangulia Nusu Fainali jana baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Mlandege SC, bao pekee la mshambuliaji wake Mzambia, Obrey Chirwa dakika ya 57 Uwanja wa Amaan.
    Nusu Fainali hiyo itakuwa sawa na marudio ya fainali ya michuano hiyo mwaka jana Uwanja wa Gombani, ambayo Azam FC iliibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Simba SC wakati huo ikiwa chini ya kocha mwingine Mbelgiji, Patrick Aussems aliyefukuzwa Desemba.
    Timu nyingine ambayo tayari imekwishatinga Nusu Fainali ni Mtibwa Sugar ya Morogoro iliyoitoa Chipukizi ya Pemba kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 1-1 jana Uwanja wa Gombani.
    Mtibwa Sugar itakutana na mshindi wa mchezo wa mwisho wa hatua ya awali leo kati ya Jamhuri ya Pemba na Yanga SC ya Dar es Salaam utakaochezwa Saa 2:15 usiku wa leo Uwanja wa Amaan.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAICHAPA ZIMAMOTO 3-1 NA KUTINGA NUSU FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI, ITAIVAA AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top