• HABARI MPYA

  Jumatano, Januari 29, 2020

  SAMATTA ‘AWAKOSAKOSA’ LEICESTER CITY, ASTON VILLA YASHINDA 2-1 NA KUTINGA FAINALI KOMBE LA LIGI ENGLAND

  Na Mwandishi Wetu, BIRMINGHAM 
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana amecheza kwa dakika 67 tu, timu yake mpya, Aston Villa ikishinda 2-1 dhidi ya Leicester City Uwanja wa Villa Park, Jijini Birmingham na kuingia fainali ya Kombe la Ligi England.
  Samatta alikuwa anacheza mechi yake ya kwanza kabisa baada ya kukamilisha uhamisho wa Pauni Milioni 8.5 kutoka KRC Genk ya Ubelgiji, klabu yake ya kwanza Ulaya aliyojiunga nayo mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Pamoja na ugeni wake, Samatta, mchezaji wa zamani wa Mbagala Market, ambayo sasa inajulikana kama African Lyon na Simba, zote za Dar es Salaam, alicheza kwa kiwango kizuri na kukaribia kufunga kabla ya kocha Dean Smith kumpumzisha dakika ya 67, akimuingiza mshambuliaji kinda wa England, Keinan Davis.
  Mbwana Samatta akisikitika baada ya kukosa bao la wazi jana Uwanja wa Villa Park, Birmingham 

  Katika mchezo huo, mabao ya Villa yalifungwa na Matt Targett dakika ya 12 na Mahmoud Ibrahim Hassan ‘Trezeguet’ dakika ya 90 na ushei tena akimalizia kazi nzuri ya Mmisri mwenzake, ist by Ahmed El Mohamady, wakati la Leicester lilifungwa na Mnigeria, Iheanacho dakika ya 72.

  Villa inaingia fainali itakayochezwa Machi 1 kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya sare ya 1-1 kwenye mchezo wa King Power Januari 8.
  Aston Villa itakutana na mshindi kati ya Manchester United na Manchester City zinazorudiana leo Uwanja wa Etihad. Mechi ya kwanza City walishinda 3-1 Old Trafford Januari 7. 
  Kikosi cha Aston Villa kilikuwa; Nyland, Konsa, Mings, Hause, Guilbert/Elmohamady dk83, Douglas Luiz, Nakamba, Targett, El Ghazi/Trezeguet dk77, Samatta/Davis dk67 na Grealish
  Leicester City: Schmeichel, Soyuncu, Evans, Chilwell, Ndidi, Ricardo Pereira, Tielemans, Maddison, Barnes/Gray dk86, Iheanacho na Perez/Vardy dk57.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA ‘AWAKOSAKOSA’ LEICESTER CITY, ASTON VILLA YASHINDA 2-1 NA KUTINGA FAINALI KOMBE LA LIGI ENGLAND Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top