• HABARI MPYA

    Monday, January 27, 2020

    TFF YAIAGIZA KAMATI YAKE YA MAADILI KUCHUNGUZA TUHUMA ZA KABWILI DHIDI YA SIMBA SC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeiagiza Kamati yake ya Maadili kufuatilia ukweli kuhusu tuhuma za upangaji matokeo zilizotolewa na kipa wa Yanga SC, Ramadhani Awamu Kabwili.
    Taarifa ya Ofisa Habari wa TFF Clfford Ndimbo leo imesema kwamba baada ya shirikisho kusikia tuhuma hizo zilizotolewa na Kabwili kupitia vyombo vya Habari, Sekretarieti imeiandikia barua Kamati yake ya Maadili kufanyia kazi suala hilo.
    TFF pia imesema itavijulisha vyombo vingine vya usalama ili visaidie uchunguzi na kuchukua hatua stahiki.

    Kipa wa tatu wa Yanga, Kabwili amenukuliwa na kituo kimoja cha Redio nchini akiishutumu klabu ya Simba kutaka kumpa hongo kwa ajili ya kufanikisha mpango wa kupanga matokeo.
    Alidai Simba ilimshawishi afanye kosa kwenye mechi dhidi ya JKT Tanzania litakalomfanya aonyeshwe kadi ya njano na kufikisha idadi ya kadi zitakazomsababisha akose mechi iliyofuata baina ya watani wa jadi katika soka ya Tanzania.
    Hata hivyo, Kabwili aliyesimama langoni kwenye mechi dhidi ya Simba SC Februari 16, mwaka jana, Yanga ikichapwa 1-0, bao pekee la mshambuliaji Mnyarwanda, Meddie Kagere dakika ya 72 amesema hakukubali kushiriki mpango huo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAIAGIZA KAMATI YAKE YA MAADILI KUCHUNGUZA TUHUMA ZA KABWILI DHIDI YA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top