• HABARI MPYA

  Ijumaa, Januari 17, 2020

  RC MAKONDA ATEULIWA KUWA MSHAURI MKUU WA BODI YA WAKURUGENZI WA SIMBA SC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameteuliwa kuwa Mshauri Mkuu wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba.
  Uteuzi huo umefanywa leo na Mwenyekiti wa Bod ya Wakurugenzi ya Mfanyabiashara Bilionea, Mohamed ‘Mo’ Dewji.
  “Nafurahi sana kumkaribisha RC wetu, Mnyama mwenzangu Paul Makonda kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya Simba akiwa kama Mshauri Mkuu (Senior Advisor). Karibu kaka. Pamoja tutajenga Simba bora zaidi! Hongera kwa uteuzi,”amesema Mo Dewji leo kwenye ukurasa wake wa Instagram.

  Na Mo Dewji amefanya uteuzi huo siku chache tangu awatikise wana Simba SC kwa kutangaza kujiuzulu usiku wa Jumatatu na kubatilisha maamuzi yake asubuhi ya Jumanne.
  Baada ya Simba SC kufungwa 1-0 na Mtibwa Sugar katika fainali ya Kombe la Mapinduzi Jumatatu usiku Uwanja wa Amaan, Zanzibar, Dewji alitangaza kujiuzulu Uenyekiti wa Bodi ya Simba SC na kubaki kama mwekezaji katika klabu hiyo kongwe Tanzania.
  Wazi Mo Dewji alikerwa na matokeo hayo, akiamini baada ya uwekezaji mkubwa Simba SC ilistahili kushinda Kombe la Mapinduzi baada ya kutolewa mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika Agosti mwaka jana.
  “Inasikitisha Simba haikushinda baada ya kulipa mishahara karibu (Sh) Bilioni 4 kwa mwaka. Najiuzulu Uenyekiti wa Bodi na nitabaki kama mwekezaji. Simba Nguvu moja. Nitaelekeza nguvu kwenye kuendeleza miundombinu na akademi ya vijana,”alisema Mo Dewji kupitia ukurasa wake wa Twitter.
  Kwa kutolewa Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na UD Songo ya Msumbiji, Simba SC ilimfuta kazi kocha Patrick Aussems aliyeifikisha timu hiyo Robo Fainali ya michuano hiyo msimu uliopita na kumuajiri Mbelgiji mwenzake, Sven Ludwig Vandenbroeck.
  Ilimuondoa pia na Msaidizi wake, Dennis Kitambi na kumuajiri Suleiman Matola pamoja na kuboresha kikosi kwa kusajili nyota wapya akiwemo Luís Jose Miquissone kutoka Msumbiji ambaye alikuwa anachezea UD Songo kwa mkopo kutoka Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
  Ikumbukwe aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu, Swedy Mkwabi alijiuzulu Septemba 14, mwaka jana miezi 10 na ushei tu tangu achaguliwe na sasa nafasi yake anakaimu aliyekuwa Mjumbe wake, Mwina Kaduguda.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: RC MAKONDA ATEULIWA KUWA MSHAURI MKUU WA BODI YA WAKURUGENZI WA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top