• HABARI MPYA

  Ijumaa, Januari 10, 2020

  KAKOLANYA APANGUA PENALTI YA KIPA MWENZAKE NA KUIPELEKA SIMBA SC FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI

  Na Mwandishi Wetu, ZANZBAR
  MLINDA mlango Beno David Kakolanya amepangua penalti ya mwisho ya Azam FC na kuipeleka Simba SC fainali ya Kombe la Mapinduzi kwa ushindi wa penalti 3-2 baada ya sare 0-0 usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Kakolanya aliye katika msimu wake wa kwanza Msimbazi tangu awasili kutoka kwa mahasimu, Yanga alipangua penalti ya kipa mwenzake, Mghana Razack Abalora.
  Awali Abalora aliokoa penalti mbili za Simba SC, kwanza ya kiungo wa kimataifa wa Sudan, Sharaf Eldin Shiboub na baadaye ya mshambulaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere.
  Waliofunga penalti za Simba SC ni beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Erasto Nyoni, mshambuliaji na Nahodha, John Bocco na kiungo Jonas Mkude.

  Waliofunga penalti za Azam FC ni mabeki Mghana, Yakubu Mohamed na Mzimbabwe Bruce Kangwa, wakati Iddi Kipagwile aligongesha mwamba wa chini, mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma akapiga juu ya lango kabla mkwaju wa Abalora kuokolewa na Kakolanya.
  Sasa Simba SC itakutana na Mtibwa Sugar ya Morogoro katika fainali ambayo iliitoa Yanga kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 1-1 jana hapo hapo Uwanja wa Amaan. 
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga/Rashid Juma, Sharaf Shiboub, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu/John Bocco na Francis Kahata/Luis Miquissone.
  Azam FC; Razack Abalora, Nicolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Abdallah Heri/Oscar Maasai, Bryson Raphael, Joseph Mahundi, Masoud Abdallah ‘Cabaye’, Shaaban Iddi Chilunda/ Abalkassim Hamisi, Obrey Chirwa/Donald Ngoma na Iddi Suleiman ‘Nado’/Iddi Kipagwile.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAKOLANYA APANGUA PENALTI YA KIPA MWENZAKE NA KUIPELEKA SIMBA SC FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top