• HABARI MPYA

  Alhamisi, Januari 16, 2020

  SIMBA SC YAENDELEA KUCHANJA MBUGA MBIO ZA UBINGWA LIGI KUU BAADA YA KUICHAPA MBAO FC 2-1

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  MABINGWA watetezi, Simba SC wamezidi kujenga matumaini ya kutetea taji lao baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Mbao FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara leo Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
  Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 38 katika mchezo wa 15, ikiendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi nane zaidi ya Coastal Union wanaofuatia kwa pointi 30 za mechi 17, wakati Azam FC ni ya tatu kwa pointi zake 29 za mechi 14.
  Hali si nzuri kwa Mbao FC inayonolewa na Kocha Mzanzibar, Hemed Suleiman ‘Morocco’, kwani baada ya kucheza mechi 17 imevuna pointi 18 tu na inashika nafasi ya 14 kwenye ligi ya timu 20.

  Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Ally Simba wa Geita aliyesaidiwa na Joseph Pombe na Makame Mdogo wote wa Shinyanga, hadi mapumziko Simba SC ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa na kiungo wake mtaalamu, Hassan Dilunga kwa shuti la umbali wa 30 na ushei dakika ya 30 baada ya kumchungulia mlinda mlango wa Mbao FC, Abdallah Makangana ‘Dida’.
  Na baada tu ya kuanza kipindi cha pili, Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck ikatanua uongozi wake kwa bao la pili lililofungwa na kiungo wake mwingine fundi, Jonas Gerald Mkude dakika ya 47 akimalizia kona ya mtaalamu mwingine, Ibrahim Ajibu.
  Mshambuliaji wa zamani wa Toto Africans na Azam FC, Waziri Junior akaifungia Mbao FC ya bao la kufutia machozi dakika ya 53 akimalizia pasi ya Herbeth Lukindo.
  Kikosi cha Mbao FC kilikuwa; Abdallah Makangana, Datus Peter, Emmanuel Charles/ Paschal Frank dk85, Babilas Chitembe, Hussein Abdallah, Chilo Mkama, Mussa Haji/Jordan John dk54, Rajab Rashid, Kauswa Bernard, Waziri Junior na Adil Sultan/ Herbeth Lukindo dk35.
  Simba SC; Beko Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Clatous Chama, Sharaf Shiboub, John Bocco, Ibrahim Ajibu/Rashid Juma dk85 na Hassan Dilunga/ Tairone Santos dk90+2.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAENDELEA KUCHANJA MBUGA MBIO ZA UBINGWA LIGI KUU BAADA YA KUICHAPA MBAO FC 2-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top