• HABARI MPYA

  Jumanne, Januari 21, 2020

  RASMI, MBWANA ALLY SAMATTA NI MCHEZAJI MPYA WA ASTON VILLA YA ENGLAND HADI 2024

  Na Mwandishi Wetu, LONDON
  KLABU ya Aston Villa ya England imekamilisha uhamisho wa mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta kwa dau la Pauni Milioni 10 kutoka klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.
  Samatta amesaini mkataba wa miaka minne na nusu, huku usajili wake ukiwa katika hatua za mwisho kukamilika wakishughulikia kibali cha kufanya kazi nchini humo.
  Kocha wa Villa, Dean Smith amesema kwamba: “Nimefurahi mno kufanikiwa kumleta Mbwana katika klabu. Amefunga mabao muda wote na ninasubiri kufanya naye kazi,”.
  Nahodha wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ni mali ya Aston Villa hadi mwaka 2024 

  Akiwa ana umri wa miaka 27 sasa, Samatta aliibukia klabu ya African Lyon wakati ikiitwa Mbagala Market ya kwao, Mbagala kabla ya kujiunga na Simba SC, zote za Dar es Salaam na baadaye TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambayo ndiyo haswa ilimkuza kisoka kabla ya kuhamia Ulaya mwaka 2016.
  Samatta amefunga mabao 76 katika mechi 191 za Genk na kwa sasa ndiye Nahodha wa timu yake ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ambayo ameifungia mabao 18 katika mechi 51. 
  Alifunga bao pekee la Genk dhidi ya Liverpool kwenye hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa mapema msimu huu Uwanja wa Anfield. 
  Samatta anatarajiwa kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ya Villa kipindi hiki ambacho inamkosa Wesley ambaye ni majeruhi na anatakiwa kuwa nje hadi mwishoni mwa msimu.
  Anakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa Villa Park mwezi huu baada ya Danny Drinkwater na Pepe Reina waliosajiliwa kwa mkopo kutoka Chelsea na AC Milan.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: RASMI, MBWANA ALLY SAMATTA NI MCHEZAJI MPYA WA ASTON VILLA YA ENGLAND HADI 2024 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top