• HABARI MPYA

  Jumatatu, Januari 13, 2020

  MO DEWJI AJIUZULU UENYEKITI WA BODI YA SIMBA SC BAADA YA KICHAPO KOMBE LA MAPINDUZI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BILONEA Mohamed ‘Mo’ Dewji amejiuzulu Uenyekiti wa Bodi ya Simba SC na kubaki kama mwekezaji katika klabu hiyo kongwe Tanzania.
  Dewji amechukua hatua hiyo mara tu baada ya mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi uliomalizika kwa Simba SC kufungwa 1-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Amaan, Zanzibar usiku huu.
  Wazi Mo Dewji amekerwa na matokeo hayo, akiamini baada ya uwekezaji mkubwa Simba SC ilistahili kushinda Kombe la Mapinduzi baada ya kutolewa mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika Agosti mwaka jana.
  “Inasikitisha Simba haikushinda baada ya kulipa mishahara karibu (Sh) Bilioni 4 kwa mwaka. Najiuzulu Uenyekiti wa Bodi na nitabaki kama mwekezaji. Simba Nguvu moja. Nitaelekeza nguvu kwenye kuendeleza miundombinu na akademi ya vijana,”amesema Mo Dewji kupitia ukurasa wake wa Twitter.
  Kwa kutolewa Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na UD Songo ya Msumbiji, Simba SC ilimfuta kazi kocha Patrick Aussems aliyeifikisha timu hiyo Robo Fainali ya michuano hiyo msimu uliopita na kumuajiri Mbelgiji mwenzake, Sven Ludwig Vandenbroeck.
  Ilimuondoa pia na Msaidizi wake, Dennis Kitambi na kumuajiri Suleiman Matola pamoja na kuboresha kikosi kwa kusajili nyota wapya akiwemo Luís Jose Miquissone kutoka Msumbiji ambaye alikuwa anachezea UD Songo kwa mkopo kutoka Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
  Ikumbukwe aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu, Swedy Mkwabi alijiuzulu Septemba 14, mwaka jana miezi 10 na ushei tu tangu achaguliwe na sasa nafasi yake anakaimu aliyekuwa Mjumbe wake, Mwina Kaduguda.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MO DEWJI AJIUZULU UENYEKITI WA BODI YA SIMBA SC BAADA YA KICHAPO KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top