• HABARI MPYA

  Jumamosi, Januari 11, 2020

  BIASHARA UNITED YAICHOMOLEA COASTAL UNION DAKIKA YA MWISHO, SARE 1-1 MKWAKWANI

  Na Mwandishi Wetu, TANGA
  BAO la dakika ya 90 na ushei la mshambuliaji Kelvin Friday limeinusuru Biashara United kulala mbele ya wenyeji, Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga leo.
  Coastal Union inayofundishwa na mchezaji wake wa zamani, Juma Ramadhani Mgunda ilitangulia kwa bao la mshambuliaji wake tegemeo la mabao, Ayoub Reuben Lyanga dakika ya 50 kabla ya mchezaji wa zamani wa Azam FC na Saint George FC ya Ethiopia kuisawazishia Biashara mwishoni mwa mchezo.
  Kwa matokeo Coastal Union inafikisha pointi 30 katika mchezo wa 17 na kuendelea kushika nafasi ya pili, nyuma ya mabingwa watetezi, Simba wenye pointi tano zaidi baada ya kucheza mechi 14 tu.

  Biashara United yenyewe inayofundishwa na kocha Mkenya, Francis Baraza inafikisha pointi 18 katika mchezo wa 17 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya 15 kwenye ligi ya timu 20.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mbeya City imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Samora mjini Iringa bao pekee la Kelvin John dakika ya 75.
  Nayo Singida United ikaichapa 1-0 Ruvu Shooting bao pekee la Elinyeswia Sumbi dakika ya 69 Uwanja  wa Liti, zamani Namfua mjini Singida.
  Polisi Tanzania ikaibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, mabao yake yakifungwa na Sixtus Sabilo dakika ya 54 na 73 kwa penalti, huku la timu ya Bukoba likifungwa na Kelvin Sabato dakika ya 60.
  Mbao FC ikalazimishwa sare ya 2-2 na JKT Tanzania mabao yake yakifungwa na Kauswa Bernard dakika ya 25 na Waziri Junior dakika ya 46 Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza, huku ya wageni yakifungwa na Shaaban Mgandila dakika ya 46 na Danny Lyanga dakika ya 50.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BIASHARA UNITED YAICHOMOLEA COASTAL UNION DAKIKA YA MWISHO, SARE 1-1 MKWAKWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top