• HABARI MPYA

  Sunday, September 17, 2017

  OKWI AFUNGA MAWILI, BOCCO MOJA, SIMBA YAUA 3-0

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imewapa burudani ya nafsi mashabiki wake leo baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Nyota wa mchezo wa leo kwa mara nyingine amekuwa mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi aliyefunga mabao mawili na kufikisha mabao sita katika mechi mbili tu za Ligi Kuu alizocheza msimu huu, kufuatia kufunga mabao manne katika ushindi wa 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye mchezo wa kwanza.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa Emmanuel Mwandembwa, aliyesaidiwa na Joseph Masija na Michael Mkongwa, hadi mapumziko Simba walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Emmanuel Okwi akishangilia baada ya kufunga mabao mawili leo dhidi ya Mwadui FC
  Emmanuel Okwi akimiliki mpira mbele ya beki wa Mwadui FC
  Mshambuliaji wa Simba, Nicholas Gyan amtoka beki wa Mwadui FC, David Luhende 
  Beki wa Mwadui FC, David Luhende akimiliki mpira mbele ya kiungo wa Simba, Shiza Kichuya  
  Mshambuliaji wa Simba, John Bocco akimtoka beki wa Mwadui FC, Abdallah Mfuko

  Bao hilo lilifungwa dakika ya saba na Okwi aliyekosa mchezo uliopita wa Simba ikitoa sare ya 0-0 na Azam Jumamosi iliyopita Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kutokana na kuchelewa kurejea baada ya kwenda kuichezea timu yake ya taifa, Uganda dhidi ya Misri mechi ya kufuzu Kombe la Dunia mwakani Urusi.
  Okwi alifunga bao hilo kwa shuti la umbali wa mita 25 baada ya kumchungulia kipa wa Mwadui, Arnold Massawe aliyekuwa amesogea mbele kidogo kufuatia pasi ya winga Shiza Kichuya aliyekuwa anacheza kama kiungo zaidi leo.
  Mwadui pamoja na kumiliki vizuri mpira walipopata nafasi, lakini hawakuwa na mipango kabisa ya kuipenya ngome imara ya Simba chini ya mabeki wa timu za taifa za Uganda na Tanzania, Juuko Murshid na Salim Mbonde.
  Kipindi cha pili nyota ya Simba iliendelea kung’ara na dakika ya 67, Okwi tena akawainua vitini mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi kwa kufunga la pili kwa shuti la umbali wa mita zisizopungua 20 baada ya pasi ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
  Mashabiki wa Simba walizomea mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mcamroon, Joseph Marius Omog mara mbili kwanza akimtoa Mghana Nicholaus Gyan na kumuingiza Mwinyi Kazimoto dakika ya 61 na baadaye akimtoa Kichuya na kumuingiza Mrundi, Laudit Mavugo dakika ya 65 wakionekana kabisa kutaka mshambuliaji John Bocco ndiye atolewe.
  Bocco akawaonyesha mashabiki wa Simba kwamba Omog alikuwa sahihi katika mabadiliko yake kwa kufunga bao la tatu dakika ya 72 kwa shuti la umbali wa mita 20 na zaidi pia. 
  Mabao yote ya Simba leo yalikuwa mazuri na yenye kudhihirisha uwezo binafasi wa wachezaji kufunga na kwa ujumla, Wekundu wa Msimbazi walikuwa katika mechi nyepesi mno jioni hii.
  Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa; Aishi Manula, Ally Shomari, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Salim Mbonde, James Kotei, Emmanuel Okwi, Muzamil Yassin/Jonas Mkude dk77, John Bocco, Nicholas Gyan/Mwinyi Kazimoto dk61 na Shiza Kichuya/Laudit Mavugo dk65.
  Mwadui FC; Arnold Massawe, Malika Ndeule, David Luhende, Revocatus Mgunga, Abdallah Mfuko, Razack Khalfan, Abdallah Seseme, Awadh Juma/Uwesu Ally dk79, Evarist Mjwahuko, Gerald Mathias/Benedicto Mwampyate dk34 na Hassan Kabunda.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: OKWI AFUNGA MAWILI, BOCCO MOJA, SIMBA YAUA 3-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top