• HABARI MPYA

    Friday, September 29, 2017

    SAMATTA: USHINDANI UMEONGEZEKA LIGI YA UBELGIJI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa KRC Genk, Mbwana Ally Samatta amesema kwamba ushindani umeongezeka katika Ligi Kuu ya Ubelgiji kwa sasa tofauti na ilivyokuwa katika misimu miwili iliyopita wakati anaingia. 
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu jana kutoka Genk, Samatta amesema kwamba timu nyingi walizokuwa wanazifunga misimu miwili iliyopita sasa zimeimarika na zinawasumbua.
    “Ni hali ya mpira wa miguu tu, kila timu imejiandaa vizuri, kwa hivyo ushindani umeongezeka, umekuwa mkubwa,”alisema Samatta baada ya kuulizwa sababu za makali ya Genk kupungua.
    Mbwana Samatta (kushoto) amesema ushindani umeongezeka katika Ligi ya Ubelgiji tofauti na ilivyokuwa wakati anaingia

    Sababu nyingi zinatajwa juu ya kupungua kwa makali ya Genk, ikiwemo mabadiliko ya benchi la Ufundi, kufuatia kuondoka kwa kocha Mbelgiji, Peter Maes aliyempokea Samatta mwaka juzi na nafasi yake kuchukuliwa na Mholanzi, Albert Stuivenberg Desemba mwaka jana na pia kuondoka kwa baadhi ya nyota wakiwemo Mnigeria Wilfred Ndidi aliyehamia Leicester City ya England na Mjamaica Leon Bailey, aliyehamia Bayer Leverkusen ya Ujerumani.
    Lakini Samatta haamini sana hayo; “Wachezaji wale waliondoka Januari na baada ya hapo tuliweza kufanya vizuri pia, japo walikuwa msaada mkubwa. Lakini naweza kusema kuna wachezaji walinunuliwa wa kariba inayofanana kwa hivyo nadhani siyo suala la kulifikiria sana,” alisema Nahodha huyo wa Tanzania.
    Katika mechi sita zilizopita ambazo KRC Genk imecheza tangu mapema Agosti, imeshinda mbili tu, ikifungwa mbili pia na sare mbili.  
    Mbwana anatarajiwa kuwasili nchini mapema wiki ijayo kujiunga na kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Malawi Oktoba 7, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. 
    Samatta amekwishacheza mechi 64 za mashindano yote tangu Januari mwaka jana alipojiunga na Genk, akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Katika mechi hizo, Samatta ambaye ni mshindi wa tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika mwaka jana alipokuwa na Mazembe, 37 alianza na mechi 24 alitokea benchi.
    Katika mechi hizo, mshambuliaji huyo wa zamani wa African Lyon, zamani Mbagala Market na Simba zote za Dar es Salaam, amefunga jumla ya mabao 21 kwenye mashindano yote.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA: USHINDANI UMEONGEZEKA LIGI YA UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top