• HABARI MPYA

    Tuesday, September 26, 2017

    YAKUBU APANIA KUFANYA MAKUBWA ZAIDI BAADA YA KUSHINDA TUZO AZAM

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BAADA ya kushinda tuzo Mchezaji Bora wa Mwezi Agosti wa Azam FC, beki Mghana Yakubu Mohammed amepania kufanya mambo makubwa zaidi kuisaidia timu hiyo.
    Yakubu ametwaa tuzo hiyo inayojulikana kama ‘NMB Player of the Month’ ikidhaminiwa na wadhamini wakuu wa timu hiyo Benki ya NMB, na anakuwa mchezaji wa kwanza wa Azam FC kuitwaa ikiwa imeanzishwa msimu huu.
    Kwa upande wa timu ya vijana ya Azam FC (Azam FC U-20) tuzo hiyo imekwenda kwa kiungo Twaha Ahmed, ambayo inadhaminiwa na wadhamini namba mbili wa timu hiyo Maji safi ya Uhai Drinking Water ikijulikana kama ‘Uhai Player of the Month’.
    Tuzo hizo za kwanza za Azam FC, zilitolewa na mgeni rasmi kwenye mchezo wetu wa jana dhidi ya Lipuli, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia.
    Akizungumza jana mjini Dar es Salaam, Yakubu aliishukuru Azam FC kwa kuanzisha tuzo hiyo akidai inaongeza ushindani kikosini pamoja na kujenga wasifu wa wachezaji (CV).
    “Tuzo hii ni nzuri kwa klabu kwa sababu nadhani kwa sasa mimi ndiye wa kwanza kuichukua msimu huu kwenye mwezi wa kwanza, hii itamfanya kila mmoja kucheza kwa kiwango cha juu na ubora kwa sababu ukishinda tuzo hii unajenga wasifu wako (CV) ni nzuri kwa kila mmoja wetu.
    “Nadhani tuzo hii ni kwa timu nzima na sio mimi pekee ni jitihada za pamoja, siwezi nikachukua mafanikio haya mwenyewe bila wachezaji wenzangu nisingeweza kushinda tuzo hii, jambo la kwanza napenda kuwashukuru wachezaji wenzangu na benchi la ufundi na kila mmoja kwenye timu, hii tuzo ni kwa ajili yetu wote na sio mimi,” alisema.
    Yakubu amekuwa sehemu ya mafanikio ya Azam FC msimu huu tokea Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ianze Agosti 26 mwaka huu, akifanikiwa kutengeneza safu bora ya ulinzi ambayo mpaka sasa haijaruhusu bao lolote kwenye mechi nne zilizochezwa akishirikiana vema na pacha wake Nahodha msaidizi Agrey Moris na kipa Razak Abalora.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YAKUBU APANIA KUFANYA MAKUBWA ZAIDI BAADA YA KUSHINDA TUZO AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top