• HABARI MPYA

  Friday, September 29, 2017

  MBARAKA: KILA MECHI NI KAMA FAINALI AZAM

  Na Mwandishi Wetu, DODOMA
  MSHAMBULIAJI tegemeo wa Azam FC, Mbaraka Yussuf amesema kwamba kila mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwao ni kama fainali.
  Mbaraka ameyasema hayo kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya wenyeji wao, Singida United katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
  Mshambuliaji huyo ameonekana kuendelea na kasi yake ya ufungaji aliyokuwa nayo msimu uliopita alipokuwa Kagera Sugar kufuatia kufunga mabao mawili katika mechi mbili mfululizo za Azam FC na kuiwezesha timu hiyo kuibuka na pointi zote tatu.
  Akizungumza leo mjini hapa, Mbaraka Yussuf alisema wanajua ya kuwa kila mchezo wanaocheza unakuwa mgumu kutokana na timu pinzani kuwakamia, lakini amedai malengo yao ni kushinda kila mtanange.
  Mbaraka Yussuf amesema kwamba kila mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwao ni kama fainali

  “Kwanza namshukuru Mungu kucheza mechi hizi salama pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kufunga pia napenda sana kujitahidi kadiri ya uwezo wangu kila mechi niwe naweza kufunga ili niweze kuweka rekodi nzuri katika msimu huu na nawaahidi mashabiki kuwa mfungaji bora,” alisema.
  Akizungumzia mchezo ujao dhidi ya Singida United, Yusuph alisema kuwa; “Kwa kweli mechi yoyote ile Azam ikikutana na timu yoyote mechi inakuwa ngumu kwa vile watu wanakuwa wanakamia sana, kauli mbiu yetu kila mechi sisi kwetu fainali tunapambana ili tuweze kufunga.”
  Azam FC ikiwa mkoani hapa Dodoma imefikia katika Hoteli ya African Dreams Conference Centre, ambapo mara ya kuwasili jana ilifanya mazoezi mepesi kwenye maeneo ya hoteli hiyo na leo Alhamisi jioni inatarajia kufanya mazoezi ya kwanza kuelekea mtanange huo unaotarajia kuwa mkali na wa aina yake.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBARAKA: KILA MECHI NI KAMA FAINALI AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top