• HABARI MPYA

  Friday, September 29, 2017

  YANGA NAYO KUCHEZA MECHI YA KIRAFIKI TABORA

  Na Adam Hando, TABORA
  CHAMA cha soka Tabora (TAREFA) kipo kwenye mazungumzo na mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,Yanga ili waende mkoani humo kucheza mchezo wa kirafiki na timu mojawapo ya klabu za huko.
  Katibu Mkuu wa TAREFA, Mhandisi Athumani Kilundumya amesema hayo zikiwa zimepita siku tano baada ya Simba kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya ‘Wana Zuke Mselebende’, Milambo FC ya Tabora pia.
  “Tumekuwa na mazungumzo na klabu ya Yanga na bado tunaendelea kuzungumza nao, ndani ya mwezi ujao tutakuwa tumepata majibu sahihi, alisema Kilundumya.
  Simba ilicheza mchezo wa kirafiki na Milambo na kutoka sare ya 0-0 ikiwa  ni mara ya pili ndani ya miezi mitano, kwani katika Pasaka ya mwaka huu, Wekundu hao wa Msimbazi walifika Tabora pia kucheza Rhino Rangers na kushinda 2-0, huku mashabiki wa Yanga wakihoji kwa nini na timu yao haifiki Tabora.
  “Msimu uliopita tulizungumza na Yanga, lakini hawakuweza kufika hapa kwani wakati ule ligi ilikuwa imekwishamalizika, ila kwa sasa wakitoka kwenye mechi zao za kanda ya ziwa kuna uwezekano wakapita mkoani hapa,”alisema Kilundumya.
  Tabora haina timu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara tangu mwaka 2013 baada ya Rhino kushuka daraja katika msimu ule ule iliopanda jambo ambalo linawanyima wakazi wa mkoa huu burudani ya soka.
  Uongozi mpya wa TAREFA ulioingia madarakani mwishoni mwa mwaka jana, uliahidi kushirikiana na klabu zao ili kuhakikisha zinapanda tena daraja kwa Rhino kwenda Ligi Kuu  na Milambo na Msange kwenda Ligi Daraja la Kwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA NAYO KUCHEZA MECHI YA KIRAFIKI TABORA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top