• HABARI MPYA

  Ijumaa, Septemba 22, 2017

  SIMBA YAMPA OKWI TUZO YA ‘SOMO KWA TFF’

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Simba SC imelipa somo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baada ya leo kumtangaza mshambuliaji wake, Mganda Emmanuel Okwi kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Agosti-Septemba, mwaka huu. 
  Hiyo inafuatia msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuanza mwishoni mwa Agosti na hakuna ajabu klabu hiyo kumtaja Mchezaji wake Bora wa mwezi ulipita mwishoni huu wa mwezi Septemba.
  Lakini TFF ilikuwa ina ujasiri wa aina yake baada ya kumtaja Okwi Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wa Agosti licha ya kwamba mwezi huo ligi hiyo ilichezwa kwa raundi moja tu.
  Mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi amekuwa Mchezaji Bora wa mwezi Agosti-Septemba mwaka huu wa klabu ya Simba 

  Simba SC wameendelea kuonyesha weledi katika tuzo zao na sasa Okwi anatajwa Mchezaji Bora wa Agosti- Septemba baada ya kuifungia timu hiyo mabao sita katika mechi tatu tu alizocheza kati ya nne ambazo klabu hiyo imecheza tangu Agosti 26.
  Okwi alifunga mabao manne katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Ruvu Shooting na akakosekana kwenye mchezo wa pili dhidi ya Azam FC kutokana na kuchelewa kurejea baada ya kwenda kuichezea timu ya yake ya taifa, The Cranes.
  Akaendeleza moto wake wa mabao katika mchezo dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga wiki iliyopita Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam akifunga mawili katika ushindi wa 3-0, kabla ya kutoka patupu jana Simba ikilazimishwa sare ya 2-2 na wenyeji, Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
  Simba wamezingatia michezo yote hiyo kumpa tuzo Okwi, lakini TFF iliona matokeo ya mechi moja tu dhidi ya Ruvu Shooting yanatosha kwa kumpa ushindi huo mchezaji huyo wa zamani wa Yanga, akiwashinda beki wa Mbao FC, Boniface Maganga na kiungo wa Mtibwa Sugar, Mohammed Issa.
  Wakati kwa ushindi wa Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligi Kuu Okwi amezawadiwa Sh. Milioni 1, Simba nayo itampa Sh. 500,000.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA YAMPA OKWI TUZO YA ‘SOMO KWA TFF’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top