• HABARI MPYA

    Sunday, September 24, 2017

    SIMBA SC YALAZIMISHWA SARE 0-0 NA MILAMBO TABORA

    Na Adam Hando, TABORA
    SIMBA SC imelazimishwa sare ya bila mabao na wenyeji, Milambo FC katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora jioni ya leo.
    Katika mchezo uliochezeshwa na mwamuzi Maulid Mwikalo kutoka mkoani Tabora, Kocha Mcameroon wa Simba SC, Joseph Marius Omog alibadili karibu kikosi kizima kutoka kile kilicholazimishwa sare ya 2-2 na Mbao FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Alhamisi wiki hii.
    Nahodha wa zamani wa Wekundu wa Msimbazi, Jonas Gerlad Mkude ndiye aliyekiongoza cha leo akicheza pamoja na Nahodha wa Rwanda, Haruna Niyonzima katikati ya Uwanja.
    Kikosi cha Simba SC kilichoanza leo Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora

    Kikosi cha Milambo FC kilichotoa sare na Simba SC leo mjini Tabora
    Kipindi cha kwanza timu hizo zilishambuliana kwa zamu, Simba ikiwatumia mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo na Juma Luizio huku ‘Wasiojulikana’ Francis Gaudence na Mrisho Kadeke wakiongoza mashambulizi ya Milambo FC.
    Kipindi cha pili Simba, Omog alibadli wachezaji watano, akimuingiza kipa wake wa kwanza, Aishi Manula kuchukua nafasi ya Emanuel Mseja, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ badala ya Juma Mwambeleko, Mwinyi Kazimoto badala ya Mohammed ‘Mo’ Ibrahim, James Kotei badala ya Muzamil Yassin, Mavugo akampisha John Bocco huku Nicholaus Gyan akichukua nafasi ya Luizo.
    Safu ya kiungo ya Milambo inayofundishwa Kocha Andrew Zoma, leo ilionyesha umahiri mkubwa ikiongozwa na ‘mafundi’ Rashid Kopa na Mfoi Nassoro waliowaonyesha kazi wazoefu wa Simba.
    Kwa ujumla Milambo inayopigana kwa juhudi zote kurejea Ligi Kuu baada ya kupotea tangu Rais wa Tanzania ni Benjamin William Mkapa, ilionyesha kiwango kizuri tofauti na matarajio Wakati Simba SC imeutumia mchezo huu kama sehemu ya maandalizi ya mchezo wake ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Stand United Oktoba 1, Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Milambo FC inajiandaa na Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara ikifungua dimba na Bulyanhulu FC ya Shinyanga wiki ijayo.
    Kikosi cha Milambo FC leo kilikuwa; Allen Steven/Katwisha Ibrahim, Hussein Mashoto, Abbas Seif/Kilawako John, Samuel Kilindi, Pius Joseph, Mfoi Nassoro, Athumani Chepe/Martin Edward, Rashid Kopa, Francis Gaudence, Mandanganya Shaabaan/Medard Mrope, Kadeke Mrisho.
    Simba SC; Emanuel Mseja/Aishi Manula, Ali Shomari, Jamal Mwambeleko/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Salim Mbonde, Yusuph Mlipili, Jonas Mkude/Said Ndemla, Mohammed Ibrahim/Mwinyi Kazimoto, Muzamil Yassin/James Kotei, Laudit Mavugo/John Bocco, Juma Luizio/Nicholaus Gyan na Haruna Niyonzima.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YALAZIMISHWA SARE 0-0 NA MILAMBO TABORA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top