• HABARI MPYA

    Wednesday, September 27, 2017

    MSUVA KUJIUNGA NA TAIFA STARS JUMATATU KWA MECHI NA MALAWI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    WINGA Simon Happygod Msuva anatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu kujiunga na kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Malawi wiki ijayo.
    Taifa Stars itamenyana na Malawi Jumamosi ya wiki ijayo na kocha Salum Shaaban Mayanga amewaita washambuliaji wake wawili tegemeo wanaocheza nje, Msuva wa Difaa Hassan El - Jadida ya Morocco na Mbwana Ally Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji. 
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Msuva amesema kwamba anatarajiwa kuwasili Dar es Salaam Oktoba 2, zikiwa ni siku tano kabla ya mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Simon Msuva anatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu kujiunga na Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi 

    “Ninashukuru nimeitwa tena timu ya taifa na tayari klabu yangu hapa imepata taarifa na nimeruhusiwa kuja nyumbani, ninatarajia kufika huko tarehe mbili (Oktoba 2, 2017)”amesema Msuva leo akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu.  
    Msuva alifanya vizuri katika mchezo uliopita wa Taifa Stars baada ya kufunga mabao yote mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Botswana Septemba 2, mwaka huu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. 
    Kuelekea mchezo na Malawi, kikosi cha Stars kinatarajiwa kuingia kambini Oktoba 1, mwaka huu kwenye Hoteli ya Sea Scape iliyoko Kunduchi, Dar es Salaam.
    Wachezaji walioitwa ni pamoja na makipa Aishi Manula (Simba SC), Ramadhani Kabwili (Yanga) na Peter Manyika (Singida United).
    Mabeki ni Gardiel Michael (Yanga), Boniphace Maganga (Mbao FC), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Kelvin Yondani (Yanga), Salim Mbonde (Simba SC), Erasto Nyoni (Simba SC) na Adeyum Ahmed (Kagera Sugar).
    Viungo ni Himid Mao ambaye pia ni Nahodha Msaidizi (Azam FC), Hamisi Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Muzamil Yassin (Simba SC), Raphael Daud (Yanga), Simon Msuva (Difaa El Jadidah/Morocco), Shiza Kichuya (Simba SC), Abdul Hilal (Tusker/Kenya) na Morel Orgenes (FC Famalicao/Ureno).
    Washambuliaji ni Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Ibrahim Hajib (Yanga) na Mbaraka Yussuph (Azam FC). 
    Benchi la Ufundi la Mayanga linaundwa na yeye mwenyewe ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Ame Ninje (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSUVA KUJIUNGA NA TAIFA STARS JUMATATU KWA MECHI NA MALAWI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top