• HABARI MPYA

    Thursday, September 28, 2017

    POULSEN AMUHAKIKISHIA NAFASI MAKAMBA NGORONGORO HEROES

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAKATI Kocha Mkuu wa timu za taifa za vijana, Kim Poulsen akitarajiwa kutangaza kikosi cha vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 - Ngorongoro Heroes, nyota wa timu hiyo Issa Abdi Makamba anaendelea vema na matibabu jijini Dar es Salaam.
    Kim Poulsen atazungumza na wanahabari kesho Ijumaa saa 5.00 asubuhi kwenye Ukumbi wa Hosteli za TFF, kuzungumzia kwa kina timu hiyo na kambi ya vijana 50 ambao atawaita kesho.
    “Vijana nitakaowataja kesho, wataingia kambini kwa wiki tatu. Muda wa siku 20 mpaka 21 unatosha kabisa kufanya mchujo wa kupata wachezaji 30 ambao wataunda kikosi kipya cha Ngorongoro Heroes,” amesema Kim.
    Issa Abdi Makamba (katikati) atakuwemo kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes

    Kocha huyo raia wa Denmark alisema: “Hata nahodha wa Serengeti Boys ana nafasi. Najua anaendelea na matibabu, lakini atakuwepo kwa sababu vijana wale wote waliounda Serengeti Boys watapewa nafasi,” amesema.
    Serengeti Boys ni timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ambayo Mei, mwaka huu ilishiriki fainali za AFCON huko Gabon ambako Makamba aliumia kabla ya kuanza kucheza.
    Akizungumzia kuhusu afya ya Makamba ambaye aliumia kidole cha mwisho katika mguu wake wa kushoto, Daktari wa timu hiyo, Shecky Mngazija, amesema: “Makamba anaendelea vema mwezi wa 10 anaweza kuanza mazoezi.”
    Mchezaji huyo yuko Dar es Salaam kwa takribani mwezi mmoja, akiishi hotelini ambako malazi na chakula - vyote kwa pamoja yanalipwa na TFF sambamba na matibabu yake.
    Matibabu ya Makamba yanasimamiwa na Dkt. Paul Marealle ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba ya TFF na Mjumbe wa Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF).
    Wakati huo huo: Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limewapa fursa mashabiki wengi kuingia uwanjani kuishangilia timu ya taifa ya wanawake wenye umri wa chini ya miaka 20 ‘Tanzanite’ itakayocheza na Falconets ya Nigeria, Jumapili Oktoba mosi, mwaka huu.
    TFF imetoa ofa katika kiingilio.
    Kiingilio kitakuwa ni Sh. 500 tu kwa mashabiki watakaoketi eneo la mzunguko huku kwa wale watakaokaa Jukwaa Kuu (VIP) watalipia Sh. 1,000 tu katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: POULSEN AMUHAKIKISHIA NAFASI MAKAMBA NGORONGORO HEROES Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top