• HABARI MPYA

  Friday, September 22, 2017

  ESPERANCE NA AL AHLY NI MECHI YA KIFO KESHO TUNISIA

  TIMU ya Esperance ya Tunisia kesho inawakaribisha Al Ahly ya Misri  katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Esperance Sportive de Tunisia watakuwa wenyeji wa Ahly ya Cairo kwenye mchezo wa marudiano wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa kesho baada ya kulazimisha sare ya 2-2 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria mwishoni mwa juma lililopita.
  Siku hiyo, Abdallah Said aliifungia bao la kwanza Al Ahly mapema tu, lakini Esperance ikajibu kwa mabao mawili mfululizo kupitia kwa Taha Yassine Khenissi na Ghailene Chaalali. 
  Walid Azaro akaisawazishia Al Ahly katikati ya kipindi cha pili na mchezo ukamalizika kwa sare ya 2-2. 
  Vigogo wa Misri wanashikilia rekodi ya kutwaa mara nyingi, mara nane taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, la mwisho wakichukua mwaka 2013.
  Esperance wametwaa taji hilo kubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Afrika mara mbili tu, mwaka 1994 na 2011. 
  Mshindi wa mchezo wa kesho atakutana na mshindi wa jumla wa mchezo kati ya Etoile du Sahel ya Tunisia na Al-Ahli Tripoli ya Libya katika Nusu Fainali.
  Esperance wanaweza kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kwenda Nusu Fainali baada ya kuvuna mabao mawili ugenini, lakini historia inawabeba Al Ahly. 
  Katika mechi saba zilizopita baina ya timu hizo mbili za Kaskazini mwa Afrika, Al Ahly imepoteza moja tu na hiyo ilikuwa ni mwaka 2011.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ESPERANCE NA AL AHLY NI MECHI YA KIFO KESHO TUNISIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top