• HABARI MPYA

    Thursday, September 28, 2017

    TASWA YALAANI KITENDO CHA CHIRWA KUMPIGA MWANDISHI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) na wahariri wa habari za michezo nchini, tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kushambuliwa kwa mwanahabari John Dande, zinazodaiwa kufanywa na straika wa Yanga, Obrey Chirwa, juzi Jumanne Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. 
    TASWA na wahariri wa habari za michezo, tunaalani tukio hilo la kushambuliwa kwa Dande ambaye ni mpigapicha wa Kampuni ya New Habari 2006 Limited, kwani kitendo hicho si cha kiungwana bali ni udhalilishaji wa taaluma ya habari na hujuma kwa tasnia na mambo kama haya  yanadhoofisha nguzo muhimu ya kujenga jamii yenye uelewa wa mambo yanayoendelea nchini na kudhoofisha mfumo wa kidemokrasia, ambao tunajitahidi kuuimarisha nchini. 
    Obrey Chirwa (wa pili kushoto) katika mzozo na Mwandishi John Dande (kulia), ambao uliingiliwa na kocha wa timu hiyo, George Lwandamina (katikati)
    Kukaa kimya, hata tukiliwazwa na kuombwa samahani kwa jambo hili, hakutatoa tafsiri nyingine kwa wana taaluma ya habari na jamii kwa ujumla isipokuwa kuliona jambo hili kama ni la kawaida. 
    Kama tukio hilo lingefanyika eneo la starehe au mitaani na mwandishi hakuwa kazini, tungelichukulia suala hilo kama faragha inayowahusu watu wawili, aliyepiga na aliyepigwa, lakini kutokana na kumtokea mwandishi akiwa kazini tena uwanjani, ndio tumelazimika kutekeleza wajibu wetu wa kuitetea taaluma na haki ya mwandishi wa habari kufanya kazi bila kusumbuliwa au vitisho.
    Kifungu cha 7 cha sheria za huduma za habari Na 12 ya mwaka 2016 kinaaainisha uhuru wa habari katika kukusanya habari kwa muktadha wa kuwepo maeneo ya matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa. Hivyo ni vyema wadau wetu wakatambua kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro.
    Tunatoa tamko hili la kulaani kitendo hicho kwa sababu sio cha kawaida hapa nchini kama ilivyo baadhi ya nchi nyingine ambazo waandishi wanapigwa na hata kuuliwa. Lakini tunachelea kulifumbia macho tukio hili kwa sababu kufanya hivyo ni kusema tunaridhika kupigwa na wachezaji na baadaye viongozi na hata mashabiki.
    TASWA na wahariri wa habari za michezo na waandishi wa habari kwa ujumla hawana na hawatakuwa na muhali na mchezaji, kiongozi au shabiki yeyote wa michezo anayefanya kitendo kama hiki, kwani huo ni uhuni na sio mwanzo mzuri na tunataka mwendo kama huu ukome mara moja na yeyote mwenye malalamiko kwa mwandishi wa habari binafsi, au chombo chake afuate taratibu za kistaarabu zilizopo.
    Hata hivyo kwa kuwa mhusika ameripoti tukio hilo kwenye vyombo vya usalama, tunawaomba waandishi wa habari wawe watulivu na waziachie mamlaka husika zitekeleze majukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi. 
    Tunaomba ushirikiano mzuri kati ya waandishi, wachezaji na viongozi wa michezo ili tucheze na tufurahie michezo kwa amani na kila mmoja aheshimu kazi ya mwenzake. Michezo iwe furaha kwa wote. Tucheze bila kupigana.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TASWA YALAANI KITENDO CHA CHIRWA KUMPIGA MWANDISHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top