• HABARI MPYA

  Monday, September 18, 2017

  KADO AREJEA KAZINI MTBWA BAADA YA KUPONA GOTI

  Na Mwandishi Wetu, MOROGORO
  BENCHI la Ufundi la Mtibwa Sugar ya Morogoro limepokea habari njema kufuatia kupona kwa kipa wake namba moja, Shaaban Hassan Kado aliyeumia mwezi uliopita.
  Kado aliumia goti baada ya kugongana na mshambuliaji wa Simba, John Bocco katika mchezo wa kirafiki Agosti 13, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na tangu hapo amekuwa nje kwa matibabu.
  Lakini akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Kado aliyerejea Mtibwa Sugar msimu huu kutoka Mwadui FC ya Shinyanga, amesema kwamba amepona kikamilifu na yupo tayari kurejea dimbani.  
  Shaaban Kado baada ya kuumia kufuatia kugongana na John Bocco Agosti 13, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam 

  Kado amesema kwamba madaktari waliokuwa wanamtibu wamemruhusu kujumuika na wachezaji wenzake kuanza mazoezi baada ya kuridhishwa na maendeleo yake.
  “Kwa kweli nimepona kabisa na niko fiti kwa ajili ya kuitumikia timu yangu, mwanzoni nilipewa ruhusa ya kufanya mazoezi mepesi, ila kwa sasa nimeanza mazoezi kikamilifu, na ninaweza kusema niko fiti kwa ajili ya mapambano,’amesema Kado.
  Kurejea kwa Kado ni habari njema kwa mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambao wana makipa wengine watatu wa kikosi cha kwanza, Abdallah Makangana ‘Dida’, Benedictor Tinocco na Abutwalib Msheri.
  Na baada ya kupona na kurejea uwanjani kwa Kado uwanjani, Mtibwa Sugar inabaki na wachezaji wawili majeruhi kikosini, ambao ni beki Hassan Isihaka ambaye tayari ameanza mazoezi mepesi na kiungo Haruna Chanongo anayesumbuliwa na maumivu ya goti pia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KADO AREJEA KAZINI MTBWA BAADA YA KUPONA GOTI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top