• HABARI MPYA

  Jumamosi, Septemba 23, 2017

  MBEYA CITY WAPANIA KUIZIMA STAND UNITED KAMBARAGE KESHO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA wa Mbeya City, Mohammed Kijuso amesema kwamba wana matumaini ya kuwafunga Stand United kwao, mjini Shinyanga kesho.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online jana mjini hapa, Kijuso alisema kwamba anatarajia mchezo mgumu kesho, lakini ana matumaini makubwa ya kushinda.
  "Ni kweli utakuwa mchezo mgumu, lakini tumejipanga kwa ajili ya kuja kushinda ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi,"amesema. 
  Mbeya City tayari ipo mjini Mbeya tangu juzi kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa ugenini wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya mechi tatu za nyumbani.
  Wachezaji wa Mbeya City wakiwa mazoezini mjini Shinyanga jana tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Stand United
  Katika mechi zake hizo tatu za awali Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, timu hiyo imeshinda mbili na kufungwa moja. 
  Ilianza kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Maji Maji ya Songea kabla ya kufungwa 1-0 na Ndanda FC na baadaye kushinda 1-0 pia dhidi ya Njombe Mji FC.
  Mbeya City itakuwa na mechi tatu Kanda ya Ziwa Victoria kuanzia kesho dhidi ya Stand United na baada ya hapo itakwenda Mwadui kucheza na Mwadui FC kabla ya kwenda Mwanza kumenyana na Mbao FC.
  Stand United imefungwa 1-0 kila mechi katika mechi zake zote tatu za awali, mbili ugenini na moja nyumbani. Ilifungwa 1-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, 1-0 na Lipuli Uwanja wa Samora mjini Iringa kabla ya kufungwa tena 1-0 na Singida United Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MBEYA CITY WAPANIA KUIZIMA STAND UNITED KAMBARAGE KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top