• HABARI MPYA

    Monday, September 18, 2017

    WACHEZAJI YANGA WAMFARIJI MANJI MAHAKAMANI, KESI YAKE NYINGINE YAAHIRISHWA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WACHEZAJI wa Yanga na benchi la Ufundi, leo wamemtembelea Mwenyekiti wao wa zamani, Yussuf Manji kumjulia hali baada ya kutoka gereza la Keko, dar es Salaam kufuatia kufutiwa mashitaka ya Uhujumu Uchumi. 
    Wachezaji hao wakiongozwa na Kocha Mkuu, Mzambia, George Lwandamina walimfuata Manji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kusutu, Dar es Salaam ambako alikwenda kusikiliza kesi yake nyingine ya tuhuma za kutumiwa dawa za kulevya.
    Pamoja na kusalimiana na kupeana mikono na wote, lakini Manji alizungumza na kirefu na Nahodha, Nadir Haroub ‘Cannavaro’. Manji alizungumza na Cannavaro akitoka mahakamani kusikiliza kesi yake, ambayo imeahirishwa hadi Septemba 25, mwaka huu.
    Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' (kulia) akizungumza na Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Yussuf Manji 
    Manji akisalimiana na makocha wa Yanga leo nje ya Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam

    Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Cyprian Mkeha Wakili wa utetezi, Hajra Mungula alisema kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kusikilizwa na wako tayari.
    Alisema mteja wake anahitaji kutoka kwa ajili ya matibabu kwa sababu yuko nje kwa dhamana, hivyo akaiomba Mahakama hiyo iisikilize kesi hiyo kwa siku tatu mfululizo.
    Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Timon Vitalis alidai kwamba anataka kusafiri mchana na hatoweza kusikiliza kesi hiyo.
    Hakimu Mkeha alisema kwamba anakwenda kwenye kikao na kuahirisha shauri hilo hadi Septemba 25 litakaposikilizwa kwa siku tatu mfululizo hadi Septemba 27.
    Ikumbukwe, Manji anadaiwa kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin kati ya Februari 6 na 9, 2017 katika eneo la Upanga Sea View Ilala alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin.
    Kesi hiyo ipo katika hatua za usikilizwaji wa mashahidi upande wa utetezi ambapo shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Mkugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Prof.Mohamed Janabi aliieleza mahakama kuwa Manji ana Vyuma kwenye moyo.
    Ikumbukwe, Alhamisi iliyopita Septemba 14, mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimuachia huru Manji baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) kumfutia mashtaka dhidi baada ya miezi miwili ya kusota rumande.
    Mbali na Manji, wengine walioachiwa huru ni Meneja Rasilimali watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda, Mtunza Stoo, Abdallah Sangey na Thobias Fwere.
    Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa wameomba 'remove order' na kwamba Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) kwa niaba ya Jamhuri wanaiarifu Mahakama kwamba hakusudii kuendelea kuwashtaki Manji na wenzake katika kesi hiyo.
    Hivyo wanaomba kuiondoa kesi hiyo chini ya kifungu cha 91(1) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
    Baada ya kueleza hayo Wakili wa Manji, Hajra Mungula ameeleza kuwa sheria inaruhusu DPP kufanya hivyo na kutokana na hatua hiyo, Hakimu Shaidi amesema kesi hiyo imefutwa na kuanzia sasa washtakiwa wapo huru.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WACHEZAJI YANGA WAMFARIJI MANJI MAHAKAMANI, KESI YAKE NYINGINE YAAHIRISHWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top