• HABARI MPYA

  Tuesday, September 19, 2017

  SIMBA YAWASILI SALAMA MWANZA TAYARI KUIVAA MBAO ALHAMISI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha Simba kimewasili salama mjini Mwanza kwa ajili ya mchezo wake ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC Alhamisi Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Simba iliyoondoka kwa ndege ya ATC mapema Alfajiri ya leo mjini Dar es Salaam imetua Mwanza na kikosi chake kamili, kasoro wachezaji wawili tu, kipa Said Mohammed Ndunda na beki Shomari Kapombe ambaoo ni majeruhi. 
  Simba imeshinda mechi zote tatu ilizokutana na Mbao FC, zikiwemo mbili za Ligi Kuu msimu uliopita Alhamisi ya Oktoba 20 iliposhinda 1-0 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na Jumatatu ya Aprili 10 iliposhindaa 3-2 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
  Mwinyi Kazimoto (kulia) na Haruna Niyonzima (kushoto) wote wapo na Simba mjini Mwanza
  Mchezo mwingine ulikuwa wa fainali ya Kombe la Azam Sports Federation Cup Mei 27, mwaka huu ambao Simba walishinda 2-1 ndani ya dakika 120 Uwanja wa Jamhuri Dodoma.
  Msimu huu Simba haitakuwa na Muivory Coast, Frederick Blagnon aliyewasaidia kushinda mechi zote dhidi ya Mbao msimu uliopita. 
  Oktoba 20, 2016; baada ya Simba kubanwa, kocha Joseph Omog alimtoa Mrundi, Laudit Mavugo na kumuingiza Blagnon aliyekwenda kutoa pasi ya bao pekee la ushindi lililofungwa na kiungo Muzamil Yassin dakika ya 86.
  Aprili 10, 2017; Baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika Simba ikiwa nyuma kwa mabao 2-0, Omog tena akamuinua Blagnon benchi kwenda kuchukua nafasi ya Juma Luizio mapema tu kipindi cha pili.
  Mbao ilipata mabao yake mapema tu kipindi cha kwanza kupitia kwa George Sangija dakika ya 21 na Evarigestus Bernard dakika ya 36.
  Blagnon akaifungia bao la kwanza la Simba dakika ya 82 kwa kichwa cha kuparaza akiwa amelipa mgongo lango la Mbao kufuatia mpira mrefu wa James Kotei na la pili dakika ya 91 baada ya kutokea purukushani kwenye eneo la Mbao kufuatia mpira mrefu wa Bokungu.
  Katika mchezo huo uliodumu kwa dakika 103 ili kufidiwa muda uliopotezwa, kiungo Muzamil Yassin ndiye aliyeifungia Simba bao la ushindi dakika ya 96 akimalizia mpira uliorudi baada ya kuokolewa na mabeki wa Mbao.
  Mei 27, 2017; Wakati timu hizo zikiwa hazijafungana hadi dakika ya 80, Omog tena anamuinua Blagnon kwenda kuchukua nafasi ya Said Ndemla na dakika 90 zikamalizika kwa sare ya 0-0 mchez ukahamia kwenye dakika 30 za nyongeza.
  Blagnon akawainua vitini mashabiki wa Simba dakika ya 95 baada ya kumzidi maarifa beki wa Mbao FC kufuatia pasi ndefu ya beki Abdi Banda, ingawa Robert Ndaki aliisawazishia Mbao dakika ya 109 akitumia makosa ya Banda aliyezubaa akidhani mfungaji kaotea.
  Refa Ahmed Kikumbo akawazawadia Simba penalti ya utata kwa madai kuna beki mmoja wa Mbao FC aliunawa mpira uliopigwa na Abdi Banda dakika 119 na winga Shiza Ramadhan Kichuya akaenda kuifungia Simba bao la ushindi.
  Hivyo Mbao watajaribu kusaka ushindi wa kwanza mbele ya Simba Alhamisi Uwanja wa CCM Kirumba. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA YAWASILI SALAMA MWANZA TAYARI KUIVAA MBAO ALHAMISI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top