• HABARI MPYA

  Sunday, September 24, 2017

  MECHI HIZI HAZIISAIDII TAIFA STARS WALA WACHEZAJI, NI KUPOTEZEANA MUDA TU

  TANZANIA itacheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Malawi Oktoba 7, mwaka huu Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam katika utaratibu wa kawaida wa kila mwezi uliowekwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
  Na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Shaaban Mayanga jana ametaja kikosi cha wachezaji 22 kwa maandalizi ya mchezo huo dhidi ya Mwale (The Flame) Jumamosi ya Oktoba 7, 2017 kuanzia Saa 10:00 jioni.
  Mayanga aliyeteuliwa Januari 4, mwaka huu kuchukua nafasi ya Charles Boniface Mkwasa, amesema kikosi kitaingia kambini Ijumaa ya Oktoba 1, mwaka huu kwenye Hoteli ya Sea Scape iliyoko Kunduchi, Dar es Salaam.
  Na wachezaji aliowaita ni pamoja na makipa Aishi Manula (Simba SC), Ramadhani Kabwili (Yanga) na Peter Manyika (Singida United), mabeki Gardiel Michael (Yanga), Boniphace Maganga (Mbao FC), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Kelvin Yondani (Yanga), Salim Mbonde (Simba SC), Erasto Nyoni (Simba SC) na Adeyum Ahmed (Kagera Sugar).
  Viungo ni Himid Mao ambaye pia ni Nahodha Msaidizi (Azam FC), Hamisi Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Muzamil Yassin (Simba SC), Raphael Daud (Yanga), Simon Msuva (Difaa El Jadidah/Morocco), Shiza Kichuya (Simba SC), Abdul Hilal (Tusker/Kenya) na Morel Orgenes (FC Famalicao/Ureno na washambuliaji Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Ibrahim Hajib (Yanga) na Mbaraka Yussuph (Azam FC). 
  Benchi la Ufundi la Mayanga linaundwa na yeye mwenyewe ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Ame Ninje (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).
  Tangu ameishika Taifa Stars, Mayanga amecheza jumla ya mechi 12, akishinda sita, sare tano na kufungwa moja tu. Bila shaka hii ni rekodi nzuri kuelekea mchezo wa 13, lakini kwanza tujiulize amecheza dhidi ya timu zipi?
  Alianza kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Botswana, akashinda 2-1 dhidi ya Burundi zote mechi za kirafiki Uwanja wa Taifa, kabla ya kwenda kulazimishwa sare ya 1-1 na Lesotho Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam katika mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
  Kutoka hapo, akaingia kwenye michuano ya Kombe la COSAFA nchini Afrika Kusini akianza na ushindi wa 2-0 dhidi ya Malawi, kabla ya kutoa sare ya 0-0 na Angola, 1-1 na Mauritius na kushinda 1-0 dhidi ya Afrika Kusini katika Robo Fainali.
  Katika mchezo wa Nusu Fainali, Tanzania ilifumuliwa 4-2 na Zambia na kuangukia kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya tatu, ambako Taifa Stars ilishinda kwa penalti 4-2 dhidi ya Lesotho baada ya sare ya 0-0.
  Kutoka hapo, timu ikaenda kutoa sare mbili mfululizo na Rwanda katika mechi za nyumbani na ugenini kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, kwanza 1-1  CCM Kirumba mjini Mwanza na baadaye 0-0 Uwanja wa Nyamirambo, Kigali hivyo Taifa Stars kutolewa kwa mabao ya ugenini.
  Mchezo wa mwisho Tanzania ilishinda 2-0 dhidi ya Botswana, ambao ulikuwa wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Katika michuano ya COSAFA, timu nyingi hupeleka vikosi vya pili, hususan timu za vijana, lakini Tanzania tulipeleka kikosi kamili, alikosekana Nahodha tu, Mbwana Samatta – maana yake pamoja na kufanya vizuri, lakini hatukupata kipimo sahihi ndiyo maana tuliporejea nyumbani tukatolewa na Rwanda katika CHAN.
  Wakati Leodegar Chilla Tenga alipokuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Taifa Stars ilikuwa inapatiwa mechi ngumu za kujipima zikiwemo dhidi ya mabingwa wa zamani wa Afrika, Cameroon, Zambia na Misri – lakini ajabu utamaduni huo umekufa ghafla baada ya beki huyo wa zamani wa kimataifa nchini kuondoka madarakani.
  Mechi ngumu zilisaidia kuijenga timu na wachezaji wetu hata viwango vyao vikapanda wakati fulani kiasi cha kuzifungia timu kama Cameroon na Morocco na hata msisimko wa soka ya nchi hii ukaanza kurudi juu.
  Lakini sasa tumerudi kwenye kucheza mfululizo na Botswana, Malawi, Burundi labda kwa lengo la kutaka matokeo mazuri kulingana na wepesi wa mechi, lakini mwisho wa siku ni mechi ambazo hazitusaidii chochote zaidi ya kuwapotezea muda wachezaji, mashabiki na kusimamisha bure tu kalenda za mashindano ya nyumbani.
  Hakuna sababu ya kutopata mechi ngumu za kujipima ili kuwajengea wachezaji wetu uwezo zaidi na kupata fursa ya kujifunza kutoka kwa wachezaji na nchi zilizo juu yetu kiuwezo – ikibidi hata kwa kusafiri kwenda ugenini badala ya kutaka lazima tucheze nyumbani, kuepuaka gharama, lakini hatupati mechi za maana.
  Rekodi ya Mayanga ni nzuri sana hadi sasa na inawafunika makocha wote wa miaka ya karibuni waliofundisha Taifa Stars, lakini aina ya mechi ambazo timu inacheza hazisaidii chochote, ni kupotezeana muda tu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MECHI HIZI HAZIISAIDII TAIFA STARS WALA WACHEZAJI, NI KUPOTEZEANA MUDA TU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top