• HABARI MPYA

    Sunday, February 07, 2021

    SIMBA SC NA AZAM FC HAKUNA MBABE DAR, WATOKA SARE YA KUFUNGANA MABAO 2-2 LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MABINGWA watetezi, Simba SC wamelazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
    Sare hiyo inaifanya Simba inayofundishwa na Mfaransa Didier Gomes Da Rosa ifikishe pointi 39 baada ya kucheza mechi 17 na kuendelea kukamata nafasi ya pili, nyuma ya watani wao wa jadi, Yanga SC wenye pointi 44 za mechi 18.
    Azam FC inayofundishwa na kocha Mzambia, George Lwandamina ‘Chicken’ inafikisha pointi 33 na inabaki nafasi ya tatu, ikiwazidi pointi nne Biashara United ya Mara baada ya timu zote kucheza mechi 18.



    Mabao yote ya Azam FC leo yamefungwa na wazawa, Iddi Suleiman ‘Nado’ na Ayoub Lyanga, wakati ya Simba yamefungwa na wageni, Mnyarwanda Meddie Kagere na Mmakonde wa Msumbiji, Luis Miquissone.
    Kiungo Mzambia, Clatous Chama aliikosesha timu yake bao dakika ya 37 baada ya mkwaju wake wa penalti kuokolewa na kipa Mganda kufuatia Miquissone kuchezewa rafu Mnyarwanda, Ally Niyonzima kwenye boksi.
    Mshambuliaji Kagere alianza kuifungia Simba SC dakika ya 27 akimalizia pasi ya kiungo Miquissone, kabla ya kiungo Iddi Nado kuisawazishia Azam FC dakika ya 67 akimalizia pasi ya mshambuliaji Mzimbabwe Prince Dube Mpumelelo.
    Kiungo Ayoub Reuben Lyanga akaifungia Azam FC bao la pili dakika ya 76 akimalizia krosi ya Iddi Nado, kabla ya Miquissone kuisawazishia Simba SC dakika ya 78 akimalizia pasi ya mshambuliaji Mkongo, Chriss Mutshimba Kope Mugalu.
    Mchezaji Bora wa Mechi ya leo ni Miquissone aliyehusika kwenye mabao yote ya Simba SC na kusababisha penalti pia ambayo Chama alikosa.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’’, Ibrahim Ame, Pascal Wawa, Thadeo Lwanga, Percet Chikwende/Bernard Morrison dk70, Rally Bwalya/Chriss Mugalu dk77, Meddie Kagere, Clatous Chama na Luis Miquissone/Muzamil Yassin dk86.
    Azam FC; Mathias Kigonya, Nico Wadada, Bruce Kangwa, Daniel Amoah, Aggrey Morris, Ally Niyonzima/Yahya Zayd dk62, Ayoub Lyanga, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Mudathir Yahya dk62, Prince Dube/Never Tigere dk90, Obrey Chirwa na Iddi Suleiman ‘Nado’.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC NA AZAM FC HAKUNA MBABE DAR, WATOKA SARE YA KUFUNGANA MABAO 2-2 LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top