• HABARI MPYA

  Saturday, February 13, 2021

  YANGA SC YACHOMOLEWA KWA PENALTI DAKIKA YA MWISHO, SARE 1-1 NA MBEYA CITY SOKOINE

  Na Mwandishi Wetu, MBEYA
  VINARA, Yanga SC wamepunguzwa kasi baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na wenyeji, Mbeya City  jioni ya leo Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
  Kwa sare hiyo, Yanga SC inafikisha pointi 45 baada ya kucheza mechi 19 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi sita zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi mbili mkononi na wastani mzuri wa mabao.
  Ilibaki kidogo tu Yanga inayofundishwa na kocha Mrundi, Cedric Kaze kuondoka na ushindi kwa bao la Deus Kaseke dakika ya 84, kama si Mbeya City kusawazisha kwa penalti dakika ya 90 na ushei kupitia kwa Pastory Athanas.
  Refa Ludovick Charles aliwapa penalti Mbeya City dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 90 kufuatia kushauriana na msaidizi wake namba mmoja, Ferdinand Chacha, wote wa Mwanza wote wakijiridhisha beki wa Yanga, Yassin Mustapha aliunawa mpira kwenye boksi.
  Na mshambuliaji Pastory Athanas akaenda kuisawazishia Mbeya City kwa mkwaju mzuri wa penalti uliompita kipa, Metacha Boniphace Mnata.


  Wachezaji wa Yanga SC waliwafuata marefa kuwazonga baada ya mchezo huo kabla ya kuzuiwa na viongozi wao akiwemo kocha Msaidizi, Nizar Khalfan. 
  Dakika 45 za kwanza za mchezo huo zilimalizika kwa timu hizo kutofungana na kipindi cha pili zikiwa zimesalia dakika sita kabla ya filimbi ya mwisho, mtokea benchi Deus Kaseke akaifungia Yanga SC bao la kuongoza.
  Zilikuwa ni juhudi binafasi za Kaseke aliyepasua katikati ya mabeki wa Mbeya City kabla ya kufumua shuti ambalo mabeki wa wenyeji walijaribu kuokolea ndani, lakini refa Ludovick Charles akawa makini.
  Kikosi cha Mbeya City kilikuwa; Haroun Mandanda, Kenneth Kunambi, Mpoki Mwakinyuki, David Mwasa, Babilas Chitembe, Edgar Mbembela, Pastory Athanas, Mathew Robert, Jean Didier/Abasarim Chidiebere dk88, Hamisi Thabit/Herbet Lukindo dk76 na Kato Yayo/Juma Shamvuni dk59. 
  Yanga SC; Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto,  Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Feisal Salum, Michael Sarpong, Fiston Abdul Razak/Ditram Nchimbi dk74 na Farid Mussa/Deus Kaseke dk67. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YACHOMOLEWA KWA PENALTI DAKIKA YA MWISHO, SARE 1-1 NA MBEYA CITY SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top