• HABARI MPYA

  Jumatano, Septemba 02, 2020

  VANDENBROECK ASHANGAZWA NA UVUMI WA KUPIGWA NA KAGERE, ASEMA HANA TATIZO NA MEDDIE

  Na Mwandishi Wetu, ARUSHA
  KOCHA Mkuu wa Simba SC, Mbelgiji Sven Ludwig Vandenbroeck ameshangazwa na uvumi kwamba yeye amegombana na mshambuliaji wake, Mnyarwanda Meddie Kagere.
  Kumekuwa na uvumi tangu jana kupitia mitandao ya kijamii, kwamba jana Kagere mfungaj wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa misimu miwili mfululizo alimpiga kocha wake mazoezini. 
  “Siwezi kutumia nguvu kwenye mambo yasiyo ya maana ambayo sijui yanatoka wapi. Mimi sina tatizo, Meddie hana tatizo, hilo ndilo ninaloweza kusema,” amesema Vandenbroeck.
  Pamoja na hayo, Mbelgiji huyo amezungumzia maandalizi ya mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Ihefu Jumapili Jijini Mbeya.

  Vandenbroeck amesema kikosi kinaendelea vizuri na maandalizi yake tangu kiwasili Jijini Mbeya jana na matarajio ni mwanzo mzuri katika Ligi Kuu.
  “Hatuna majeruhi, kila mmoja yupo sawa, kila mmoja yupo tayari kucheza, hivyo nina nafasi ya kuchagua kati ya wachezaji 29,”amesema.
  Ligi Kuu inatarajiwa kuanza Jumapili na mbali ya Simba kuwa wageni wa Ihefu iliyopanda Ligi Kuu msimu huu Uwanja wa Sokoine kuanzia Saa 10:00 jioni – watani wao wa jadi, Yanga SC watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons ya Mbeya kuanzia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
  Mechi nyingine za Jumapili, Namungo FC watawakaribisha Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, Mtibwa Sugar watawakaribisha Ruvu Shooting Uwanja wa CCM Gairo mkoani Morogoro.
  Wageni wengine katika Ligi Kuu, Dodoma Jiji FC watawakaribisha Mwadui FC Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, Biashara United watawakaribisha Gwambina FC waliopanda Ligi Kuu msimu huu pia Uwanja wa Karume Musoma mkoani Mara.
  Mechi za kwanza za Ligi Kuu zitakamilishwa Jumatatu kwa KMC kuwaalika Mbeya City Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, Kagera Sugar kuwa wenyeji wa JKT Tanzania Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera na Azam FC kuwakaribisha Polisi Tanzania Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: VANDENBROECK ASHANGAZWA NA UVUMI WA KUPIGWA NA KAGERE, ASEMA HANA TATIZO NA MEDDIE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top