• HABARI MPYA

  Ijumaa, Septemba 25, 2020

  SAMATTA AONDOKA ASTON VILLA, AJIUNGA NA FENERBAHCE YA UTURUKI KWA MKOPO WA MWAKA MMOJA

  Na Mwandishi Wetu, ISTANBUL 
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amejiunga na Fenerbahce ya Uturuki kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Aston Villa ya England.
  Kwa mujibu wa Express & Star, Samatta mwenye umri wa miaka 27 anakwenda kucheza Uturuki kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu atakapouzwa moja kwa moja kwa ada ya Pauni Milioni 5.5 kumalizia mkataba wake wa Villa.
  “Nafahamu Fenerbahce ni klabu kubwa kiasi gani. Siyo tu Uturuki, klabu inayofahamika na kubwa duniani,”amesema Samatta na kuongeza; "Nina furaha kuwa hapa katika familia hii kwa sababu itakuwa changamoto mpya na kubwa kwangu.
  "Fenerbahce ina mashabiki wengi na wakati wote wanataka kushinda. Nami pia nataka kushinda. Nimekuja kwa ombi hili, nina furaha sana na ninatumai tutashinda mataji mengi,”amesema.

  Mbwana Samatta amejiunga na Fenerbahce kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Aston Villa 

  Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Tanzania usajili wake unaweza kukamilishwa kwa wakati na kuuwahi mchezo dhidi ya mahasimu, Galatasaray Jumapili.
  Samatta alijiunga na Aston Villa Januari mwaka huu kwa dau la Pauni Milioni 10 kutoka klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji akisaini mkataba wa miaka minne na nusu.
  Amecheza mech 14 tu hadi sasa na kufunga mabao mawili – Aston Villa ikichapwa 2-1 na wenyeji, AFC Bournemouth mechi ya Ligi Kuu alifunga kwa kichwa dakika ya 70 Uwanja wa Vitality.
  Siku hiyo AFC Bournemouth iliyomaliza pungufu baada ya Jefferson Lerma kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 51, ilitangulia kwa mabao ya kiungo wa kimataifa wa Denmark, Philip Billing dakika ya 37 na beki Mholanzi, Nathan Ake dakika ya 44.
  Samatta akafunga tena bao la kufutia machozi Aston Villa ikichapwa 2-1 na Manchester City katika fainali ya Kombe la Ligi England Uwanja wa Wembley Jijini London.
  Manchester City inayofundishwa na kocha Mspaniola, Pep Guardiola ilitangulia kwa mabao ya mshambuliaji wake tegemeo, Muargentina Sergio Aguero dakika ya 20 akimalizia pasi ya Philip Foden na Rodri Hernandez akimalizia pasi ya İlkay Gundogan dakika ya 30.
  Akiwa ana umri wa miaka 27 sasa, Samatta aliibukia klabu ya African Lyon wakati ikiitwa Mbagala Market ya kwao, Mbagala kabla ya kujiunga na Simba SC, zote za Dar es Salaam na baadaye TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambayo ndiyo haswa ilimkuza kisoka kabla ya kuhamia Ulaya mwaka 2016. 
  Akiwa Genk, Samatta ambaye sasa ndiye Nahodha wa Taifa Stars, alifunga mabao 76 katika mechi 191 hadi Aston Villa kuvutiwa naye na kumnunua.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA AONDOKA ASTON VILLA, AJIUNGA NA FENERBAHCE YA UTURUKI KWA MKOPO WA MWAKA MMOJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top