• HABARI MPYA

  Jumapili, Septemba 20, 2020

  CHAMA APIGA MBILI MABINGWA WATETEZI, SIMBA SC WAITANDIKA BIASHARA UNITED 4-0 DAR

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM

  MABINGWA watetezi, Simba SC wameibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Biashara United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzana Bara usiku wa leo Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

  Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi saba baada ya kucheza mechi tatu na kurejea nafasi ya pili, nyuma ya Azam FC yenye pointi tisa ikiwazidi kwa wastani wa mabao, mahasimu, Yanga SC.

  Nyota wa mchezo wa leo kwa mara nyingine amekuwa kiungo Mzambia, Clatous Chota Chama aliyefunga mabao mawili kipindi cha kwanza.

  Chama aliye katika msimu wake wa tatu tangu asajiliwe Simba SC kutoka Lusaka Dynamos ya kwao, Zambia alifunga bao la kwanza dakika ya tisa akimalizia pasi ya kiungo wa kimataifa wa Msumbiji, Luis Miquissone.


  Kiungo Mzambia, Clatous Chama amefunga mabao mawili Simba SC ikiiibuka na ushindi 4-0 dhidi ya Biashara United leo

  Chama, mchezaji wa zamani wa ZESCO United ya kwao, Zambia na Al Ittihad ya Misri akafunga bao la pili dakika ya 26 akimalizia pasi ya kiungo mpya kutoka Power Dynamos ya kwao, Zambia, Rally Bwalya.

  Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Tanzana Bara kwa misimu miwili mfululizo iliyopita, mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere akafunga bao la tatu dakika ya 52 akimalizia pasi ya Miquissone.

  Chama akapokea pasi ya winga Mghana, Bernard Morrison aliyetokea benchi na kumpasia mshambuliaji mpya, Mkongo Chriss Mugalu aliyefunga bao la nne dakika ya 84.

  Mechi zilizotangulia, Azam FC imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Mbeya bao pekee la kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Ally Niyonzima dakika ya 25 Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya. 

  Nayo Coastal Union ikalazimishwa sare ya bila kufungana na Dodoma Jiji FC Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga. 

  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Joash Onyango, Pascal Wawa, Gerson Fraga/ Said Ndemla dk46, Luis Miquissone, Muzamil Yassin, Meddie Kagere/Chriss Mugalu dk76, Rally Bwalya/Bernard Morisson dk72 na Clatous Chama.

  Biashara United; Daniel Mgore, Ally Kombo/ Omary Banda dk70, Deogratius Judika, Tariq Simba, Kelvin Friday, Mpapi Nassib, Mustapha Batozi, Lenny Kissu, Abdulmajid Mangaro na Omary Nassoro. 

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: CHAMA APIGA MBILI MABINGWA WATETEZI, SIMBA SC WAITANDIKA BIASHARA UNITED 4-0 DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top