• HABARI MPYA

    Sunday, September 06, 2020

    MO DEWJI, WAZIRI KIGWANGALLA, KILOMONI NA UWEKEZAJI SIMBA SC

    Na Luqman Maloto, DAR ES SALAAM
    KWANZA, Kigwangalla na Kilomoni wote ni Hamis. Sema, Kigwangalla ni Hamis mwenye cheo. Waziri. Kilomoni ni Hamis veterani wa soka. Staa wa zamani wa Simba, aliyebeba zege kujenga jengo la klabu, Msimbazi, Kariakoo, Ilala, Dar es Salaam. Kilomoni ni Simba sana.
    Hamis wote; Kilomoni na Kigwangalla, katika nyakati tofauti wameibuka na hoja ya kuhoji uwekezaji Simba wa hisa asilimia 49 unaofanywa na bilionea MO Dewji. Uwekezaji wenye thamani ya Sh20 bilioni.
    Hamis ambaye ni Simba sana, Kilomoni, alikuwa wa kwanza kutaka mchanganuo wa thamani ya klabu uwe wazi ili MO asiilalie klabu. Vilevile alitaka Sh20 bilioni za uwekezaji zitoke mapema.

    Tangu lini maskini akawa na sauti mbele ya tajiri? Kilomoni akajikuta peke yake. Ile siku aliyotaka kufanya mkutano na waandishi wa habari Kinondoni Block 41, akabebwa na polisi. Toka siku hiyo, Kilomoni kawa mkimya. Hahoji, haulizi.

    Jana, Hamis Kigwangalla aliibuka mtandaoni, "twitani', akaanza kuhoji uwekezaji wa MO Simba. Kigwangalla anauliza mbona Sh20 bilioni hazijatoka?
    Kilomoni alipohoji uwekezaji wa MO Simba, sababu iliyomuongoza ni mchakato na mazingira ya uwekezaji.
    Kigwangalla anapohoji uwekezaji wa MO Simba, sababu inayomuongoza ni uteuzi wa Barbara Gonzalez kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Simba.
    Kilomoni alisukumwa na uwekezaji ndani ya Simba, akahoji uwekezaji, akafungua mpaka shauri mahakamani. Alionekana mpinga mabadiliko Simba. Ukweli ni kuwa Kilomoni alikuwa akipigania kile ambacho aliona ni haki ya Simba. Na si dhambi mtu kupigania anachokiamini.
    Kigwangalla ameshitushwa na Simba kumteua Barbara kuwa CEO. Akahoji wasifu wake wa kitaaluma na uzoefu wa kazi (CV). Akaambatanisha na taarifa kuwa Barbara amekuwa msaidizi binafsi wa MO, vilevile mtendaji mkuu wa taasisi ya MO, inayoitwa MO Dewji Foundation.
    Hivyo, Kigwangalla hakupata msukumo wa kuhoji uwekezaji wa MO Simba mpaka Barbara alipoteuliwa kuwa CEO wa klabu. Halafu, kipindi Kilomoni anahoji uwekezaji Simba, Kigwangalla alikuwa kimya.
    Tena, zipo rekodi, Kigwangalla alikuwa mgeni rasmi kwenye matukio makubwa ya Simba. Utoaji wa tuzo za MO kwa wachezaji wa Simba, bila kusahau mechi ya Simba dhidi ya TP Mazembe. Je, Kigwangalla hakuwa na tatizo la uwekezaji wa MO Simba mpaka Barbara alipoteuliwa kuwa CEO?
    Pengine kuna mtu alijiandaa kuuliza; Kigwangalla ana shida gani na Barbara? Mbona alikuwa mchungu aliposikia kateuliwa kuwa CEO?
    Atakuwepo wa kushangaa; mbona huko nyuma Kigwangalla alionekana muunga mkono uwekezaji wa MO Simba na hata kushiriki matukio kama mgeni rasmi, lakini sasa kageuka?
    Tweet ya MO, ikatanua goli. MO alionekana kuumizwa na tweet ya Kigwangalla, aliyeandika kuwa kuna siku atapigwa mawe kwa sababu anafanya ujanjaunja Simba. MO akasema sio vizuri binadamu kumuombea mwenzio apigwe mawe.
    Mwishoni MO hakumaliza kiungwana, akasema: "Pia nisamehe, mkopo wa pikipiki ulioniomba haikuwezekana." Ukisoma maneno ya MO, unaona anajaribu kuufikishia umma wa Watanzania kuwa tatizo la Kigwangalla sio Barbara kupewa u-CEO, bali ni nongwa ya kunyimwa mkopo wa pikipiki.
    Maneno hayo saba ya MO "Pia nisamehe, mkopo wa pikipiki ulioniomba haikuwezekana", yamesababisha Kigwangalla aijibu tweet ya MO mara tatu, akiambatanisha majibu tofauti.
    Mosi, Kigwangalla pamoja na kumtaka MO aeleze kama ameshalipa Sh20 bilioni, aliandika: "Ningekuwa nilikuomba rushwa au msaada ningeona aibu, lakini kukopa, kila mtu anakopa. Hata wewe una mikopo."
    Pili, Kigwangalla akaandika: "Nilikuomba unikopeshe pikipiki kwa mwezi mmoja tu ukashindwa pamoja na kujinasibu wewe ni bilionea. Kama ulishindwa kunikopesha pikipiki 25 kwa mwezi mmoja, utaweza kulipa Sh20 bilioni za Simba?"
    Tatu, Kigwangalla akashusha lingine: "Ulivyo huna maadili ya biashara, mtu anakukopa faragha, unabanwa kwa hoja, unaingiza mashambulizi binafsi, unakwepesha na kumtangaza. Unataka na mimi niseme mambo yako binafsi hadharani? Au watu/benki waliokukopesha wakutangaze? Sema suu uone!"
    Hizo tweets tatu, Kigwangalla amejibu tweet moja ya MO. Halafu Kigwangalla akatweet mkataba wa uwekezaji Simba, kutaka watu wajionee kwamba MO hatimizi vigezo vya uwekezaji.
    MO; hakupaswa kutangaza kuwa Kigwangalla alimuomba mkopo. Yalikuwa mambo ya kibiashara na yanapaswa kubaki chini ya zulia la kibiashara.
    Hapa nakubaliana na Kigwangalla kuwa MO hana maadili ya kibiashara. Nafahamu lengo la MO lilikuwa kutuambia kuwa Kigwangalla anamchukia kwa sababu alimnyima mkopo wa pikipiki. Je, ni maadili gani kutangaziana siri za kibiashara?
    Kigwangalla; jibu la kwanza kuwa sio aibu kukopa kwani hata yeye MO ana mikopo, lilitosha kabisa. Kitendo cha Kigwangalla kuijibu tena na tena tweet moja ya MO, kilionesha kweli suala la pikipiki lilimuuma sana.
    Kisaikolojia, majibu mengi ya Kigwangalla yanatuambia kuwa "anajihisi kuaibishwa na MO", kwa hiyo anapambana kuifuta aibu. Ndio maana kila jibu analotoa, anaona halitoshi, anaandika lingine na lingine.
    Laiti Kigwangalla angepata utulivu kidogo tu, angebaini kuwa MO ndiye alijiabisha kuingiza suala la mkopo wa pikipiki katika sakata la uwekezaji Simba na uteuzi wa Barbara kuwa CEO.
    Kwa hatua ya sasa, MO na Kigwangalla wote wamejichoresha. MO ameonekana ana "uchanga" mwingi. Tutaogopa kukopa kwake, maana hakawii kutangaza. Kigwangalla ameonesha ana kitu binafsi na MO ndio maana anampinga sasa.
    Madaktari wana dawa ambazo huziita "truth serum". Hutumika kumpumbaza mtu ili aseme ukweli aliokusudia kuuficha. Uteuzi wa Barbara umekuwa ni truth serum katikati ya MO na Kigwangalla. Hatimaye wamecheua nongwa na vinyongo vyao. Tumejua.
    Kigwangalla naye ni Simba. Kuna mtu aliniuliza, kwani akina Hamis wa Simba wana tatizo gani na MO? Nikamjibu mbona MwanaFA naye ni Hamis wa Simba lakini hana tatizo na MO?
    Mwingine akasema Hamis Kingwangalla ni HK na Hamis Kilomoni ni HK. Je, ma-HK wa Simba wana nongwa gani na MO? Nikamjibu, hata Hamis Kisiwa, Mkurugenzi wa Wanachama Simba naye ni HK, lakini hana noma na MO.
    Mtoto wangu akauliza, je, Barbara anaiweza kazi? Nikamjibu, kama Barbara anazodolewa kwa uanamke wake ni dhambi kubwa ya kijinsia ambayo inafanyika. Hakuna aliyeweza kazi bila kukabidhiwa kazi na kupewa nafasi huru ya kuitenda kazi.
    Mashabiki wa Simba kulaumu Barbara kuwa CEO kwa kuitukuza CV ya Senzo aliyedakwa na Yanga ni kudhihirisha kuwa Yanga wamewapiga panapouma.
    Waliomwajiri Senzo kwa kusoma CV yake, ndio waliomwajiri Barbara baada ya kukaa naye na kuona uwezo wake. Kama walikuwa sahihi kwa Senzo kwa nini tusiamini wapo sahihi kwa Barbara?
    Usimponde mtu usiyeujua uwezo wake. Angalau Barbara amekuwepo kwenye michakato yote ya mabadililo ya Simba, anajua ilipotoka, ilipo na inapotakiwa kwenda.
    Wapo wanaoponda kuwa Barbara hana wasifu mkubwa katika uongozi wa soka. Sheikh, Barbara ni CEO wa kampuni, sio mkurugenzi wa ufundi wa timu. Yeye aachwe ajenge utawala na biashara za timu, ufundi utashughulikiwa na mafundi.
    (Makala hii imeandikwa na Luqman Maloto, anayepatikana kwa kwenye mitandao yote ya kijamii kama @luqmanmaloto)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MO DEWJI, WAZIRI KIGWANGALLA, KILOMONI NA UWEKEZAJI SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top