• HABARI MPYA

  Jumatatu, Septemba 28, 2020

  SAMATTA AINGIA KIPINDI CHA PILI FENERBAHCE YALAZIMISHWA SARE YA 0-0 NA GALATASARAY

  Na Mwandishi Wetu, ISTANBUL 

  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku wa Jumapili ametokea benchi kipindi cha pili, timu yake mpya, Fenerbahce ikilazimishwa sare ya 0-0 na Galatasaray katika mchezo wa Ligi Kuu ya Uturuki Uwanja wa Telekom Jijini İstanbul.

  Samatta aliyeejiunga na Fenerbahce juzi kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Aston Villa ya England – aliingia uwanjani dakika ya  66 kuchukua nafasi ya Mame Baba Thiam.

  Samatta, mwenye umri wa miaka 27 atacheza Uturuki kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu atakapouzwa moja kwa moja kwa ada ya Pauni Milioni 5.5 kumalizia mkataba wake wa Villa.


  Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Tanzania alijiunga na Aston Villa Januari mwaka huu kwa dau la Pauni Milioni 10 kutoka klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji akisaini mkataba wa miaka minne na nusu.

  Amecheza mech 14 tu hadi sasa na kufunga mabao mawili – Aston Villa ikichapwa 2-1 na wenyeji, AFC Bournemouth mechi ya Ligi Kuu alifunga kwa kichwa dakika ya 70 Uwanja wa Vitality.

  Siku hiyo AFC Bournemouth iliyomaliza pungufu baada ya Jefferson Lerma kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 51, ilitangulia kwa mabao ya kiungo wa kimataifa wa Denmark, Philip Billing dakika ya 37 na beki Mholanzi, Nathan Ake dakika ya 44.

  Samatta akafunga tena bao la kufutia machozi Aston Villa ikichapwa 2-1 na Manchester City katika fainali ya Kombe la Ligi England Uwanja wa Wembley Jijini London.

  Manchester City inayofundishwa na kocha Mspaniola, Pep Guardiola ilitangulia kwa mabao ya mshambuliaji wake tegemeo, Muargentina Sergio Aguero dakika ya 20 akimalizia pasi ya Philip Foden na Rodri Hernandez akimalizia pasi ya İlkay Gundogan dakika ya 30.

  Akiwa ana umri wa miaka 27 sasa, Samatta aliibukia klabu ya African Lyon wakati ikiitwa Mbagala Market ya kwao, Mbagala kabla ya kujiunga na Simba SC, zote za Dar es Salaam na baadaye TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambayo ndiyo haswa ilimkuza kisoka kabla ya kuhamia Ulaya mwaka 2016. 

  Akiwa Genk, Samatta ambaye sasa ndiye Nahodha wa Taifa Stars, alifunga mabao 76 katika mechi 191 hadi Aston Villa kuvutiwa naye na kumnunua.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA AINGIA KIPINDI CHA PILI FENERBAHCE YALAZIMISHWA SARE YA 0-0 NA GALATASARAY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top