• HABARI MPYA

  Friday, September 18, 2020

  MTIBWA SUGAR YAPATA USHINDI WA KWANZA LIGI KUU, YAWACHAPA IHEFU 1-0 PALE PALE SOKOINE

  Na Mwandishi Wetu, MBEYA                          

  BAO pekee la mshambuliaji Jaffar Salum Kibaya dakika ya 35 limetosha kuipa ushindi wa 1-0 Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Ihefu SC Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.

  Huo unakuwa ushindi wa kwanza kwa Mtibwa Sugar ya kocha Zubery Katwila baada ya sare mbili mfulilizo katika mechi zake mbili za awali, nyumbani mkoani Morogoro.

  Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Polisi Tanzania imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na JKT Tanzania Uwanja wa Ushirika, Moshi mkoani Kilimanjaro.

  Daruwesh Saliboko alianza kuifungia Polisi Tanzania dakika ya 32, lakini Kelvin Kongwe Sabato akaisawazishia JKT Tanzania dakika ya 64 na sasa kila timu imeshinda mechi moja, imefungwa moja na sare moja katika michezo yake mitatu hadi sasa.


  Raundi ya tatu ya Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi mbili, Kagera Sugar wakiwakaribisha Yanga SC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Tanzania Prisons wakiwa wenyeji wa Namungo FC Uwanja wa Mandela, Sumbawanga.

  Kesho kutwa mabingwa watetezi, Simba SC watamenyana na Biashara United ya Musoma mkoani Mara na Coastal Union wataikaribisha Dodoma Jiji Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, wakati Mbeya City watamenyana na Azam.

  Raundi ya tatu itakamilishwa Jumatatu kwa michezo mingine miwili, Ruvu Shooting na Gwambina Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani na Mwadui FC watawakaribisha KMC Uwanja wa Mwadui Complex,  Shinyanga.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MTIBWA SUGAR YAPATA USHINDI WA KWANZA LIGI KUU, YAWACHAPA IHEFU 1-0 PALE PALE SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top