• HABARI MPYA

  Jumamosi, Septemba 05, 2020

  VANDENBROECK ASEMA HATARAJII MTEREMKO KWA IHEFU FC KESHO UWANJA WA SOKOINE

  Na Mwandishi Wetu, MBEYA
  WAKATI Ligi Kuu ya Tanzania Bara inatarajiwa kuanza kesho, kocha Mkuu wa Simba SC, Mbelgiji Sven Ludwig Vandenbroeck amesema hatarajii mteremko mbele ya wenyeji, Ihefu FC waliopanda msimu huu, mchezo ambao utafanyika Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya. 
  Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Mbeya leo, Vandenbroeck amesema kwamba siku zote mechi ya kwanza ya Ligi huwa ngumu, kwa sababu kila timu inataka kuanza vyema.
  “Sisi tumejiandaa na wachezaji wote ambao tumekuja nao Mbeya wapo tayari kwa mchezo. Tumejipanga kufanya kazi yetu ikiwezekana kuwashinda na kuanza ligi na alama tatu,” amesema Vandenbroeck.
  Kocha Mbelgiji wa Simba SC, Sven Ludwig Vandenbroeck amesema hatarajii mteremko mbele ya Ihefu FC kesho
  Kikosi cha Simba SC kimefanya mazoezi ya mwisho leo Uwanja wa Sokoine kabla ya kuivaa Ihefu FC kesho
  Ligi Kuu inatarajiwa kuanza kesho na mbali ya Simba kuwa wageni wa Ihefu iliyopanda Ligi Kuu msimu huu Uwanja wa Sokoine kuanzia Saa 10:00 jioni – watani wao wa jadi, Yanga SC watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons ya Mbeya kuanzia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
  Mechi nyingine za Jumapili, Namungo FC watawakaribisha Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, Mtibwa Sugar watawakaribisha Ruvu Shooting Uwanja wa CCM Gairo mkoani Morogoro.
  Wageni wengine katika Ligi Kuu, Dodoma Jiji FC watawakaribisha Mwadui FC Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, Biashara United watawakaribisha Gwambina FC waliopanda Ligi Kuu msimu huu pia Uwanja wa Karume Musoma mkoani Mara.
  Mechi za kwanza za Ligi Kuu zitakamilishwa Jumatatu kwa KMC kuwaalika Mbeya City Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, Kagera Sugar kuwa wenyeji wa JKT Tanzania Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera na Azam FC kuwakaribisha Polisi Tanzania Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: VANDENBROECK ASEMA HATARAJII MTEREMKO KWA IHEFU FC KESHO UWANJA WA SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top