• HABARI MPYA

  Jumamosi, Septemba 26, 2020

  MEDDIE KAGERE, WAWA NA MUGALU WOTE WAFUNGA SIMBA SC YAITANDIKA GWAMBNA FC 3-0 DAR

  Na Mwandishi Wetu, SUMBAWANGA

  MABINGWA watetezi, Simba SC wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Gwambina FC 3-0 usiku wa leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

  Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 10 baada ya kucheza mechi nne, sasa ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Azam FC inayoongoza kwa pointi zake 12.

  Simba SC ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza 1-0 kwa bao la mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, mzaliwa wa Uganda, Meddie Kagere dakika ya 39 akimalizia pasi ya kiungo kutoka Msumbiji, Luis Miquissone.


  Dakika tano baada ya kuanza kipindi cha pili, beki Muivory Coast, Serge Pascal Wawa akaifungia Simba SC bao la pili kwa shuti la mpira wa adhabu, baada ya kiungo mpya, Mzambia Rally Bwalya kuangushwa umbali wa mita 30. 

  Mshambuliaji mpya, Mkongo Chris Mutshimba Kopa Mugalu aliyekuchukua nafasi ya Kagere kipindi cha pili, akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 90 na ushei akimalizia pasi ya mtokea benchi mwenzake, winga Mghana, Bernard Morrison.

  Gwambina kutoka Misungwi mkoani Mwanza iliyopanda Ligi Kuu msimu huu inakamilisha mechi nne bila ushindi, ikifungwa tatu na kutoa sare moja.

  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Azam FC imerejea kileleni baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, wahamiaji Tanzania Prisons, bao la Mzimbabwe, Prince Mpumeled Dube dakika ya 90 Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa.

  Nayo Polisi Tanzania imeibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC, mabao ya Marcel Kaheza dakika ya 11 na 61 na Tariq Seif dakika ya 33 Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa Ruvu Shooting kuwa wenyeji wa Biashara United Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Mwadui FC na Ihefu Uwanja wa Mwadui Complex, Kishapu mkoani Shinyanga na Mtibwa Sugar na Yanga SC Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

  Raundi ya Nne ya Ligi Kuu itakamilishwa Jumatatu kwa mchezo mmoja tu, Coastal Union wakiwa wenyeji wa JKT Tanzania kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.

  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Joash Onyango, Paschal Wawa, Said Ndemla, Clatous Chama/ Jonas Mkude dk5, Muzamil Yassin, Meddie Kagere/Chriss Mugalu dk75, Rally Bwalya/ Benard Morrison dk67 na Luis Miquissone.

  Gwambina FC; Mohamed Makaka, Aaron Lulambo/ Hamad Nassor dk50, Amos Kadikilo, Novaty Lufunga, Baraka Mtuwi, Yussuf Kagoma, Japhet Mayunga, Yussuf Lwenge, Paul Nonga, Jacob Massawe na Rajab Athumani. 

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MEDDIE KAGERE, WAWA NA MUGALU WOTE WAFUNGA SIMBA SC YAITANDIKA GWAMBNA FC 3-0 DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top