• HABARI MPYA

  Jumamosi, Septemba 12, 2020

  SIMBA SC YAPUNGUZWA KASI LIGI KUU BAADA YA KULAZIMISHWA SARE YA 1-1 NA MTIBWA SUGAR MORO

  Na Mwandishi Wetu, MOROGORO
  MABINGWA watetezi, Simba SC wamepunguzwa kasi baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
  Sare hiyo ni ya kwanza kwa Simba SC inayofundishwa na Mbelgiji Sven Ludwig Vandenbroeck katika mchezo wa pili tu wa msimu, ikitoka kushinda 2-1 ugenini dhidi ya wageni katika Ligi Kuu, Ihefu FC Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
  Kwa Mtibwa Sugar huo ni mwendelezo wa matokeo yasiyovutia tangu msimu ulioptia chini ya kocha Zubery Katwila, kwani kabla ya leo, pia walitoka kutoa 0-0 na Ruvu Shooting ya Pwani kwenye mchezo wao wa kwanza Uwanja wa CCM Gairo, hapo hapo Morogoro. 


  Ulikuwa mchezo mzuri na wa ushindani zaidi, Simba SC wakipata bao lao mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kucheza vizuri tangu mwanzo na Mtibwa Sugar wakisawazisha mwanzoni mwa kipindi cha pili na wakaendelea kucheza vizuri hadi mwisho. 
  Kiungo Muzamil Yassin alianza kuifungia Simba SC dakika ya 45 akiiadhibu timu yake ya zamani kwa shuti kali kutoka upande wa kulia wa Uwanja ambalo kipa Mzanzibar, Abdultwalib Mshery alilitemea nyavuni.
  Lakini Mtibwa Sugar ikasawazisha bao hilo dakika ya 46 kupitia kwa kiungo wake mshambuliaji, Boban Zilintusa aliyemchambua kwa kichwa kipa namba moja Tanzania, Aishi Salum Manula. 
  Mechi nyingine za leo, Dodoma Jiji FC iliichapa JKT Tanzania 2-0, mabao ya Jamal Mtegeta dakika ya 50 na Dickson Ambundo dakika ya 80 Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
  KMC imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam. Mabao ya KMC yamefungwa  na Hassan Kabunda dakika ya 21 na Kenneth Masumbuko dakika ya 85, wakati la Prisons limefungwa na Kassim Mdoe dakika ya 39. 
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi tatu; Ihefu itawakaribisha Ruvu Shooting kuanzia Saa 8:00 mchana Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya, Biashara United watamenyana na Mwadui FC kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Karume Musoma mkoani Mara na baadaye Saa 1:00 usiku, vigogo Yanga SC watamenyana na Mbeya City Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
  Jumatatu kutakuwa na mchezo mmoja tu wa kukamilisha Raundi ya pili, Namungo FC wakiwaalika Polisi Tanzania kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.
  Kikosi cha Mtibwa Sugar kilikuwa; Abdultwalib Mshery, Salum Kanoni, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Geoffrey Luseke, Dickson Job, Baraka Majogoro, Haroun Chanongo, Juma Nyangi, Ibrahim Ahmada Hilika/Salum Kihimbwa dk78, Boban Zirintusa/Ally Yussuf Makarani dk61na Joseph Mkele Jojo/Jaffar Salum Kibaya dk68
  Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Joash Onyango, Kennedy Willson, Jonas Mkude, Bernard Morrison/Meddie Kagere dk67, Muzamil Yassin/Francis Kahata dk77, John Bocco, Clatous Chama na Luis Miquissone. 


  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAPUNGUZWA KASI LIGI KUU BAADA YA KULAZIMISHWA SARE YA 1-1 NA MTIBWA SUGAR MORO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top