• HABARI MPYA

  Jumapili, Septemba 06, 2020

  SIMBA SC WAANZA VYEMA KUTETEA UBINGWA WA LIGI KUU, WAICHAPA IHEFU SC 2-1 SOKOINE

  Na Mwandishi Wetu, MBEYA
  MABINGWA watetezi, Simba SC wameuanza vyema msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu SC iliyopanda daraja katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
  Nahodha na mshambuliaji John Raphael Bocco alianza kuwafungia Wekundu wa Msimbazi dakika ya 11 akimalizia pasi nzuri ya kiungo Mghana, Bernard Morrison.
  Mchezaji wa zamani wa Ndanda FC ya Mtwara, Omary Mponda akaifungia Ihefu SC bao la kusawazisha dakika ya 15 akimalizia pasi ya Willy Mgaya.
  Muzamil Yassin akaifungia Simba SC bao la ushindi dakika ya 43 akimalizia pasi ya kiungo mwenzake, Mzambia Clatous Chotta Chama.


  Refa Martine Saanya akakataa mabao mawili kwa ushauri wa wasaidizi wake, Jesse Erasmo wote wa Morogoro na Janeth Balama wa Iringa, yote wakitafsiri wafungaji walikuwa wameotea, Mponda dakika ya 47 upande wa Ihefu na mtokea benchi Meddie Kagere wa Simba dakika ya 74. 
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Khamis Mcha ‘Vialli’ dakika ya 69 liliwapa ushindi wa 1-0 Dodoma Jiji FC dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
  Nayo Mtibwa Sugar ikalazimishwa sare ya bila kufungana na Ruvu Shooting ya Mlandizi, Pwani Uwanja wa CCM Shabiby, Gairo mkoani Morogoro.
  Mechi za mchana; Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi bao pekee la Bigirimana Blaise dakika ya 64 lilitosha kuwapa wenyeji, Namungo FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
  Na Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara – bao pekee Kelvin Friday dakika ya 88 likawapa ushindi wa 1-0 Biashara United dhidi ya Gwambina FC ya Misungwi mkoani Mwanza.
  Kikosi cha Ihefu kilikuwa; Andrew Kayuni, Omary Kindamba, Emmanuel Kichiba/Paul Materazzi dk90, Geofffrey Raphael, Michael Masinda, Soud Mlindwa, Jordan John/Samuel Jackson dk65, Willy Mgaya, Joseph Kinyozi, Omary Mponda na Enock Jiah/ Teps Evans dk78.  
  Simba SC; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Joash Onyango, Keneddy Willson, Jonas Mkude, Hassan Dilunga/Ibrahm Ajibu dk67, Muzamil Yassin, John Bocco, Clatous Chama na Bernard Morrison/Meddie Kagere dk67.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC WAANZA VYEMA KUTETEA UBINGWA WA LIGI KUU, WAICHAPA IHEFU SC 2-1 SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top