• HABARI MPYA

    Saturday, September 26, 2020

    PRINCE DUBE AFUNGA DAKIKA YA MWISHO AZAM YAICHAPA PRISONS 1-0 NA KUREJEA KILELENI LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, SUMBAWANGA

    TIMU ya Azam FC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, wahamiaji Tanzania Prisons jioni ya leo Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa.

    Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, mshambuliaji mpya kutoka Zimbabwe, Prince Mpumeled Dube dakika ya 90 akimalizia kwa kichwa krosi iliyochongwa na winga aliyetokea benchi kipindi cha pili, Idd Suleiman 'Nado' kutoka upande wa kushoto.

    Na kwa ushindi huo, Azam FC inafikisha pointi 12 baada ya mechi nne ikirejea kileleni, wakati Tanzania Prisons inabaki na pointi zake nne baada ya mechi pia.


    Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Polisi Tanzania imeibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC, mabao ya Marcel Kaheza dakika ya 11 na 61 na Tariq Seif dakika ya 33 Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

    Polisi Tanzania inafikisha pointi saba, wakati Dodoma FC iliyopanda Ligi Kuu msimu huu inabaki na pointi zake saba baada ya timu zote kucheza mechi nne hadi sasa.

    Mechi nyingine ya Ligi Kuu inafuatia Saa 1:00 usiku wa leo kati ya mabingwa watetezi, Simba SC na Gwambina FC Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam.

    Ligi Kuu itaendelea kesho kwa Ruvu Shooting kuwa wenyeji wa Biashara United Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Mwadui FC na Ihefu Uwanja wa Mwadui Complex, Kishapu mkoani Shinyanga na Mtibwa Sugar na Yanga SC Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

    Raundi ya Nne ya Ligi Kuu itakamilishwa Jumatatu kwa mchezo mmoja tu, Coastal Union wakiwa wenyeji wa JKT Tanzania kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.

    Kikosi cha Tanzana Prisons kilikuwa; Jeremiah Kisubi, Michael Mpesa, Benjamin Asukile, Vedastus Mwihambi, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil, Salum Kimenya/Jeremiah Juma dk40, Lambert Sibiyanka, Mohamed Mkopi, Kassim Mdoe/Ramadhan Ibata dk72 na Gasper Mwaipasi/Ezekia Mwashilindi dk60. 

    Azam FC; David Mapigano, Nico Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohamed, Abdallah Kheri, Ally Niyonzima/Mudathiri Yahaya dk40, Never Tigere/ Idd Nado dk61, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Prince Dube, Richard D’jodi/ Obrey Chirwa dk61 na Ayoub Lyanga.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PRINCE DUBE AFUNGA DAKIKA YA MWISHO AZAM YAICHAPA PRISONS 1-0 NA KUREJEA KILELENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top