• HABARI MPYA

  Jumanne, Septemba 22, 2020

  SAMATTA JUKWAANI ASTON VILLA IKIANZA VYEMA LIGI KUU ENGLAND, YAICHAPA SHEFFIELD UNITED 1-0

  Na Mwandishi Wetu, BIRMINGHAM 

  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta hakuwepo hata benchi, timu yake Aston Villa ikiichapa 1-0 na Sheffield United katika mchezo wa Ligi Kuu ya England Uwanja wa Villa Park Jijini Birmingham.

  Hii ni mara ya kwanza Samatta akiwa fiti tangu asajiliwe Aston Villa Januari mwaka huu anakosekana hata benchi – na inaongeza uvumi kwamba hayumo tena kwenye mipango ya klabu na ataondolewa kabla ya dirisha kufungwa.

  Bao peke la Aston Villa jana lilifungwa na Ezri Konsa Ngoyo dakika ya 63 akimaliza pasi ya bek mwenzake Tyrone Mings.


  Sheffield United ilicheza pungufu ya mchezaj mmoja jana tangu dakika ya 12 baada ya John Egan kutolewa kwa kadi nyekundu kufuatia kumchezea rafu mshambuliaji mpya, Ollie Watkins.

  Kipa mpya wa Aston Villa, Emiliano Martinez aliyesajlwa kutoka Arsenal alifanya kazi nzuri mno jana ikiwemo kuokoa mchomo wa hatari wa John Lundstram.

  Samatta alijiunga na Aston Villa Januari mwaka huu kwa dau la Pauni Milioni 10 kutoka klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji akisaini mkataba wa miaka minne na nusu.

  Amecheza mech 14 tu hadi sasa na kufunga mabao mawili – Aston Villa ikichapwa 2-1 na wenyeji, AFC Bournemouth mechi ya Ligi Kuu alifunga kwa kichwa dakika ya 70 Uwanja wa Vitality.

  Siku hiyo AFC Bournemouth iliyomaliza pungufu baada ya Jefferson Lerma kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 51, ilitangulia kwa mabao ya kiungo wa kimataifa wa Denmark, Philip Billing dakika ya 37 na beki Mholanzi, Nathan Ake dakika ya 44.

  Samatta akafunga tena bao la kufutia machozi Aston Villa ikichapwa 2-1 na Manchester City katika fainali ya Kombe la Ligi England Uwanja wa Wembley Jijini London.

  Manchester City inayofundishwa na kocha Mspaniola, Pep Guardiola ilitangulia kwa mabao ya mshambuliaji wake tegemeo, Muargentina Sergio Aguero dakika ya 20 akimalizia pasi ya Philip Foden na Rodri Hernandez akimalizia pasi ya İlkay Gundogan dakika ya 30.

  Akiwa ana umri wa miaka 27 sasa, Samatta aliibukia klabu ya African Lyon wakati ikiitwa Mbagala Market ya kwao, Mbagala kabla ya kujiunga na Simba SC, zote za Dar es Salaam na baadaye TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambayo ndiyo haswa ilimkuza kisoka kabla ya kuhamia Ulaya mwaka 2016. 

  Akiwa Genk, Samatta ambaye sasa ndiye Nahodha wa timu yake ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, alifunga mabao 76 katika mechi 191 hadi Aston Villa kuvutiwa naye na kumnunua.

  Tayari vyombo vya Habari vimeripoti kwamba klabu za West Bromwich Albion ya England pia na Fenerbahce ya Uturuki zinawania saini ya Samatta.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA JUKWAANI ASTON VILLA IKIANZA VYEMA LIGI KUU ENGLAND, YAICHAPA SHEFFIELD UNITED 1-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top