• HABARI MPYA

  Thursday, January 22, 2015

  STARS MABORESHO SARE 1-1 NA RWANDA KIRUMBA

  Na Mahmoud Zubeiry, MWANZA
  TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23, maarufu kama Taifa Stars Maboresho imetoka sare ya kufungana bao 1-1 na Rwanda katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza jioni ya leo.
  Licha ya kuundwa na wachezaji vijana wadogo, lakini timu ya Mholanzi, Mart Nooij ilicheza soka ya kuvutia, hususan kipindi cha pili dhidi ya Rwanda iliyoundwa na wazoefu, wakiwemo wachezaji wa kulipwa. 
  Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Rwanda wakitangulia dakika ya tisa na Tanzania kusawazisha dakika ya 44.
  Bao la Rwanda lilifungwa na Jean Baptiste Mugiraneza kwa kichwa akiunganisha krosi ya Emery Bayisenga aliyemtoka Gardiel Michael.
  Kevin Friday akishangilia baada ya kuifungia Stars bao la kusawazisha leo dhidi ya Rwanda
  Nahodha wa Rwanda, Haruna Niyonzima Niyonzima akimuacha chini Simon Msuva wa Stars
  Simon Msuva wa Stars akimtoka Jean Baptiste Mugiraneza leo

  Tanzania walisawazisha kupitia kwa Kevin Friday dakika ya 44 aliyefumua shuti kali nje kidogo ya 18 baada ya kupata pasi nzuri ya kichwa ya Simon Msuva, ambaye naye alipokea pasi ya Miraj Adam.
  Rwanda inayofundishwa na kocha wa muda, Muingereza Lee Johnson ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi wa FERWAFA, walitawala mchezo kipindi cha kwanza na ilionekana kama Tanzania ingefungwa mabao zaidi, lakini uimara wa safu ya ulinzi iliyoongozwa na kipa Peter Manyika ulisaidia.
  Kipindi cha pili, Stars Maboresho iliimarika zaidi na kuuteka mchezo, ikipeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Rwanda, kiasi cha kukosa mabao mawili ya wazi.
  Mashabiki zaidi ya 15,000 waliojitokeza Uwanja wa CCM Kirumba wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kwa ujumla walionekana kufurahishwa na kiwango cha timu hiyo, inayoandaliwa kwa ajili ya mechi za kufuzu za CHAN.
  Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Peter Manyika, Miraj Adam, Gardiel Michael, Andrew Vincent, Joram Mgeveke, Salim Mbonde, Said Ndemla, Hassan Dilunga, Kevin Friday/Rashid Mandawa dk70, Simon Msuva na Shiza Ramadhani/Salum Telela dk45.
  Rwanda; Olivier Kwizera, Emery Bayisenga, Ismail Nshyutamagara, Maxime Sekamana/Yanick Mukunzi dk75, Michael Rusheshangonga, Jean Baptiste Mugiraneza, Haruna Niyonzima, Issa Bigiramana/Andrew Buteera dk61, Betrand Iradukunda/Justin Mico dk90, Patrick Sibomana na Janvier Mutuima. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: STARS MABORESHO SARE 1-1 NA RWANDA KIRUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top