• HABARI MPYA

  Saturday, January 24, 2015

  MRWANDA AWAPA RAHA YANGA SC

  Na Mahmoud Zubeiry, MOROGORO
  YANGA SC imekaa mguu sawa katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Uwanja wa Jamhuri, Morogoro jioni ya leo.
  Yanga SC sasa inapanda nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kutimiza pointi 18 za mechi 10, nyuma ya mabingwa watetezi, Azam FC wenye pointi 20.
  Shukrani kwake, mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Danny Davis Mrwanda aliyefunga bao hilo dakika ya 42 akimalizia mpira uliorudi baada ya kipa Tony Kavishe kupangua krosi ya Simon Msuva.
  Mpira uliozaa bao hilo, ulianzia kwa Sherman ambaye aliangushwa nje kidogo ya boksi na Haruna Niyonzima akaenda kumuanzia haraka Simon Msuva aliyemtoka beki Fanuel Simon na kutia krosi ya bao lililofungwa na Mrwanda, aliyesajiliwa Desemba Yanga SC kutoka Polisi.
  Yanga SC ilicheza vizuri kipindi cha kwanza, lakini ugonjwa wa kukosa mabao ya wazi ulijirudia kabla ya Mrwanda kuupatia tiba mwishoni mwa kipindi hicho. 
  Danny Mrwanda kulia akikimbia kushangilia baada ya kuifungia Yanga SC bao pekee la ushindi leo

  Awali, refa Ahmada Simba wa Kagera alitaka kuwapa bao la utata Yanga SC dakika ya 13 baada ya piga nikupige langoni mwa Polisi ambayo mwishowe ilionekana kama mpira umevuka mstari wa goli, lakini msaidizi wake namba moja, John Kanyenye wa Mbeya akasema halikuwa bao.
  Wachezaji wa Yanga SC walimfuata refa kumlalamikia pamoja kocha wao, Mholanzi Hans van der Pluijm, kabla ya mchezo kuendelea.  
  Kipindi cha pili, Polisi walibadilika na kuanza kulitia misukosuko lango la Yanga SC, hadi kocha Pluijm akaamua kurekebisha ukuta wake, akimtoa Kevin Yondan na kumuingiza Rajab Zahir.
  Kiungo wa Yanga SC, Andrey Coutinho akiwatoka wachezji wa Polisi
  Kipa Tony Kavishe wa Polisi, akidaka mpira katikati ya washambuliaji wa Yanga SC, Danny Mrwanda kulia na Simon Msuva kushoto. Mwingine ni beki wake, Chacha Marwa akiwa tayari kutoa msaada

  Makali ya Polisi kipindi cha pili yalichangiwa na kuingia kwa mshambulaji wa Yanga anayecheza kwa mkopo timu ya jeshi la Polisi Morogoro, Said Bahanuzi.
  Bahanuzi alikuwa mwiba kwa ukuta wa Yanga SC wakati wote kipindi cha pili na mara mbili alikaribia kufunga.
  Kikosi cha Polisi FC kilikuwa; Tony Kavishe, Mohammed Mpopo, Simon Fanuel, Chacha Marwa, Laban Kamboole, Lulanga Mapunda, Nahoda Bakari, Said Mkwangu, Imani Mapunda, Six Mwakasega/Said Bahanuzi dk48 na Suleiman Kassim ‘Selembe’.
  Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kevin Yondan/Rajab Zahir dk56, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Telela, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Hassan Dilunga dk72, Kpah Sherman, Danny Mrwanda na Andrey Coutinho/Hussein Javu dk80.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MRWANDA AWAPA RAHA YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top