• HABARI MPYA

  Friday, January 23, 2015

  ‘VITOTO’ VYA MABORESHO VIMEIHENYESHA RWANDA ILIYOUNDWA NA NYOTA WA KOMBE LA DUNIA

  Na Mahmoud Zubeiry, MWANZA
  MKAKATI wa maboresho ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars- jana umeonekana kupiga hatua baada ya timu hiyo kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Rwanda katika mchezo wa kirafiki, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
  Haikuwa sare tu inayotia matumaini ya mkakati huo, bali soka nzuri iliyoonyeshwa na vijana wadogo, ambao ndiyo kwanza wanakomazwa katika soka ya Tanzania.
  Hapana shaka, baada ya filimbi ya kuhitimisha mchezo huo, Rwanda walifurahia matokeo, kwa sababu walikaribia kupoteza mechi hiyo.
  Kikosi cha Rwanda kilichocheza na Taifa Stars Maboresho jana kina wachezaji watano waliocheza Kombe la Dunia la U17 Mexico mwaka 2011

  Mshambuliaji chipukizi wa Tanzania, Simon Msuva alikosa bao la wazi akiwa amebaki na kipa wa Rwanda, Olivier Kwizera kipindi cha pili, ambalo labda lingekuwa la ushindi kwa Stars kama angefunga.
  Piga nikupige mbili za hatari zilitokea langoni mwa Amavubi, lakini wakafanikiwa kuokoa na kuanza kulaumiana wenyewe kwa kuruhusu hali hiyo.
  Mashabiki waliojitokeza kwa wingi kiasi Uwanja wa Kirumba waliondoka kurejea makwao nafsi zao zikiwa ‘swafi’ kwa kuridhishwa na uwezo wa timu na wachezaji kwa ujumla.
  Vijana hao walikutana na timu ya taifa kamili ya Rwanda kwa sasa, inayoundwa na wachezaji wenye uzoefu wa kutosha, ambao baadhi yao walicheza Fainali za Kombe la Dunia za vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2011 nchini Mexico.
  Baada ya kufika Nusu Fainali za U17 za Afrika nyumbani, Kigali, watoto wa Rwanda walikwenda Mexico na kupangwa kundi gumu, C pamoja na England, Uruguay na Canada na wakafanikiwa kutoa sare moja, wakifungwa michezo miwili.
  Walifungwa 2-0 na England, 1-0 na Uruguay kabla ya kwenda sare ya 0-0 na Canada- na kutoka vijana waliocheza mechi hizo za Mexico, watano walikuwapo Uwanja wa Kirumba jana ambao ni mabeki Michel Rusheshangoga, Emery Bayisenge aliyekuwa Nahodha, viungo Andrew Buteera na Janvier Benedata Mutuima na mshambuliaji Justin Mico.
  Lakini pia katika kikosi cha Amavubi jana chini ya kocha wa muda, Muingereza Lee Johnson ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA), walikuwepo wachezaji wazoefu kama Ismail Nshyutamagara, Maxime Sekamana, Yanick Mukunzi, Jean Baptiste Mugiraneza, Haruna Niyonzima, Issa Bigiramana, Betrand Iradukunda na Patrick Sibomana.
  Jean Baptiste Mugiraneza ni mcheaji mzoefu Rwanda, hapa anamuacha chini Simon Msuva wa Taifa Stars Maboesho
  Kikosi cha Taifa Stars Maboresho kinaundwa na chipukizi ambao ndiyo kwanza wanakomazwa katika soka ya Tanzania

  Hiki ni kikosi cha Rwanda ambacho hata ilipokuwa ikiitwa Taifa Stars ile tunayoita ‘full mziki’, kilikuwa kinaifunga timu yetu, lakini jana kimetulizwa na makinda kama Peter Manyika, Miraj Adam, Gardiel Michael, Andrew Vincent, Joram Mgeveke, Salim Mbonde, Said Ndemla, Hassan Dilunga, Kevin Friday, Simon Msuva na Shiza Ramadhani.
  Katika mchezo huo, hadi mapumziko, timu hizo tayari zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Rwanda wakitangulia dakika ya tisa na Tanzania kusawazisha dakika ya 44.
  Bao la Rwanda lilifungwa na Jean Baptiste Mugiraneza akiunganisha kwa kichwa krosi ya Emery Bayisenga aliyemtoka Gardiel Michael.
  Tanzania walisawazisha kupitia kwa Kevin Friday dakika ya 44 aliyefumua shuti kali nje kidogo ya 18 baada ya kupata pasi nzuri ya kichwa ya Simon Msuva, ambaye naye alipokea pasi ya Miraj Adam.
  Tayari kocha Mholanzi, Mart Nooij amesema anawaandaa vijana hao kwa ajili ya mechi za kufuzu kwa Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, ambayo itafanyika nchini Rwanda mwaka 2016.
  Baada ya matokeo ya jana, timu hiyo inahitaji programu nzuri ya maandalizi, ili muda utakapowadia wa mechi za kufuzu za CHAN, iwe imara zaidi.
  Sare nyumbani si matokeo ya kujivunia, kuelekea mechi za mtoano za nyumbani na ugenini, lakini kutoka kufungwa nyumbani na Burundi mfululizo hadi matokeo ya jana, ukweli ni kwamba timu ya Maboresho imepiga hatua.  
  Ni mkakati ambao ulianza kwa kusuasua, lakini kwa sasa unaelekea kutoa dira mpya ya soka ya Tanzania.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ‘VITOTO’ VYA MABORESHO VIMEIHENYESHA RWANDA ILIYOUNDWA NA NYOTA WA KOMBE LA DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top