• HABARI MPYA

  Jumatano, Januari 28, 2015

  NDOA YA FKF - KPL YAVUNJIKA KENYA

  Na Vincent Malouda, NAIROBI
  NDOA baina ya Shirikisho la Soka la Kenya, FKF na Kampuni inayosimamia ligi kuu nchini humo, KPL, imevunjika rasmi mchana wa leo baada ya kutoelewana kuhusu mfumo wa ligi kuu kwanzia msimu ujao.
  FKF ilipendekeza ligi kuu iwe na jumla ya timu 18 huku KPL wakipuuzilia mbali pendekezo hilo na kusisitiza kuwa ligi iwe na timu 16 ilivyokuwa misimu iliyopita.
  Malumbano hayo yaliendelea kwa takribani miezi miwili sasa huku wakilishirikisha Shirikisho la Soka duniani, FIFA ambapo wadau wake walipendekeza mashirika yote ielewane, jambo ambalo halijazaa matunda kufikia leo.

  Katika taarifa kwa vyombo vya habari, FKF ilisema imevunja rasmi mazungumzo hayo na sasa ligi kuu itakuwa na timu 18 na itang’oa nanga tarehe 14 Februari huku KPL nao wakihabarisha kuwa ligi itasalia na timu 16 na itaanza tarehe 21 Februari.
  “Tunasikitika kutangaza kuwa FKF imevunja mazungumzo baina yake na KPL kuhusu kuongeza idadi ya timu zitakazoshiriki ligi kuu msimu ujao,” ujumbe huo ulisoma.
  “Kufuatia hilo, FKF imeamua ligi kuu itakuwa na timu 18 na itajulikana kama FKF Premier League vilabu vyote vikipata milioni 9 shilingi za Kenya kwa msimu kutoka kwa wadhamini.”
  KPL kwa upande wao waliwakashifu FKF kwa kupuuza agizo la FIFA ambalo inasemekana liliegemea timu 16 huku ikitangaza msimamo wake.
  “KPL haitajihusisha tena na mjadala wowote na FKF kuhusu swala hili na itazidi kuheshimu sheria na msimamo wa FIFA.”
  Kakamega Homeboyz na Nakumatt FC zingejiunga na timu 16 kwenye ligi kuu ili kuafikia pendekezo la FKF la vilabu 18.
  Habari hizi si nzuri kwa timu zinazojiandaa kwa msimu ujao unaofaa kuanza mwezi ujao huku wapenzi wa soka wakihamaki kwenye mitandao ya kijamii.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NDOA YA FKF - KPL YAVUNJIKA KENYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top