• HABARI MPYA

  Ijumaa, Januari 30, 2015

  NGOMA INOGILE MATAIFA YA AFRIKA, NANI KUJISOGEZA KWA MWALI WIKIENDI HII?

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika kesho zinaingia katika hatua ya Robo Fainali, huku vigogo kama Cameroon, Senegal, Mali, Afrika Kusini na Zambia vikirejea nyumbani mapema baada ya mechi za makundi.
  Lakini kigogo mmoja kati ya wawili, anayetabiriwa kubeba Kombe lililoachwa wazi na Nigeria ambao hawakufuzu kwenye fainal za mwaka huu, anatarajiwa kung’oka wikiendi hii wakati Algeria itakapomenyana na Ivory Coast.
  Mechi hiyo itakayochezwa Jumapili mjini Malabo baina ya timu mbili ambazo zilicheza Kombe la Dunia mwaka huu Brazil inatarajiwa kuwa ya ‘kukata na shoka’.
  Ghana, kigogo mwingine wa Afrika aliyekuwa Brazil miezi sita iliyopita, atacheza na Guinea mjini Malabo mapema siku hiyo katika mchezo wa kwanza.
  Awali, kesho Jumamosi, wenyeji Equatorial Guinea watakuwa na mtihani mzito mbele ya Tunisia mjini Bata baada ya mechi ya upinzani mkali ya majirani, Kongo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Awali, mechi hizo ilikuwa zichezwe katika miji midogo ya Ebibeyin na Mongomo, lakini zimehamishwa kwa sababu za kiusalama na pia hali ya viwanja kuwa si nzuri.
  Ivory Coast na Algeria zitamenyana Jumapili mjini Malabo

  Algeria, nchi ya Afrika inayoongoza katika viwango vya ubora wa soka vya FIFA, imeendelea kufanya vizuri kwa miezi 12 sasa katika soka ya kimataifa, ikiwemo kupelekana hadi dakika za nyongeza na Ujerumani katika 16 Bora ya kombe la Dunia. 
  Tangu hapo, wameshinda mechi tano kati ya sita za kufuzu AFCON na pia wakashinda mechi za kundi lao dhidi ya Afrika Kusini na Senegal.
  Lakini Ivory Coast, ambayo imeanza taratibu mashindano ya mwaka huu, kabla ya kuitoa Cameroon katika mchezo wa mwisho Jumatano, sasa wanaonekana kuimarika.
  Guinea iliipiku Mali na kutinga Robo Fainali baada ya kushinda bahati nasibu katika zoezi lililofanyika mjini Malabo jana.
  Bahati nasibu ilitumika kuamua mshindi wa pili wa Kundi D kufuatia timu zote kulingana kwa kila kitu baada ya mechi zao tatu za makundi. Ivory Coast iliyomaliza na pointi tano imeongoza Kundi.
  Sare tatu mfululizo za 1-1 kwa timu zote zilimaanisha haziwezi kutenganishwa kwa pointi, wala mabao na baada ya Guinea kufuzu kwa sarafu sasa itamenyana na Ghana Jumapili mjini Malabo.
  Ni timu mbili tu, kati ya nane zilizofika Robo Fainali mwaka huu, ambazo na katika fainali zilizopita pia mwaka 2013 nchini Afrika Kusini zilifika hatua hiyo, nazo ni Ghana na Ivory Coast.
  Ghana iliitoa Cape Verde kwa kuichapa 2-0, mabao ya Wakaso dakika ya 54 kwa penalti na 90+5, wakati Ivory Coast iling’olewa na Nigeria walioibuka mabingwa kwa kuchapwa 2-1.
  Safari ya Ghana katika fainali za mwaka juzi iliishia katika Nusu Fainali walipotolewa na Burkina Faso kwa penalti 3-2 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 120.
  Je, timu zipi zitapenya Nusu Fainali AFCON baada ya mechi za wikiendi hii? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.

  Tembelea link hii kwa taarifa zaidi za michezo bofya hapa

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NGOMA INOGILE MATAIFA YA AFRIKA, NANI KUJISOGEZA KWA MWALI WIKIENDI HII? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top